• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
VROOOM! hatimaye,hatimaye

VROOOM! hatimaye,hatimaye

MBIVU na mbichi kuhusu Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari rally itajulikana baada ya siku nne ya mtihani mkali kwa madereva 58 utakaoanza rasmi hii leo.

Wakiongozwa na bingwa mara saba duniani Sebastien Ogier, madereva kutoka Ufaransa, Uingereza, Ubelgiji, Estonia, Finland, Japan, Italia, Norway, Bolivia, Czech, Poland, Uganda na Kenya, wataondoka jukwaani mmoja baada ya mwingine nje ya Jumba la KICC asubuhi leo.

Wataelekea kituo cha kimataifa cha michezo cha Kasarani kufanya mkondo maalum wa kilomita 4.84 saa sita adhuhuri.Kisha, madereva watasafari hadi Naivasha baadaye leo kulala huko kabla ya kuraukia kupaisha magari yao umbali wa kilomita 129.78 kupitia barabara za mashindano za Chui Lodge (13.34km), Kedong (32.68km) na Oserian (18.87km).

Jumamosi watafanya jumla ya kilomita 132.08 katika maeneo ya Elementaita (14.67km), Soysambu (20.33km) na Sleeping Warrior (31.04km).Mashindano haya yaliyopata umaarufu kama magumu duniani miaka iliyopita na yanayorejea kwenye WRC tangu 2002, yatakamilika Jumapili. 4

Siku ya mwisho, madereva watapaisha mashine zao katika maeneo ya Loldia (11.33km), Hell’s Gate (10.56km) na Malewa (9.71km). Barabara kadhaa zitarudiwa kufikisha mikondo 18 kabla ya kukamilika katika eneo la Hell’s Gate.

Wapenzi wa mbio za magari wameruhusiwa na serikali kujitokeza katika maeneo waliotengewa kuyatazama mashindano haya yatakayoshuhudia barabara kubwa za Mombasa-Nairobi, Nakuru-Eldoret, Nakuru-Kericho, Nakuru-Nyahururu, Narok-Mai Mahiu-Naivasha pamoja na Kikopey-Elementaita, zikifungwa siku tofauti.

Mashabiki wameonywa dhidi ya kukiuka masharti makali ya afya kudhibiti virusi vya corona.Mfaransa Ogier, ambaye amekalia juu ya jedwali ya msimu huu baada ya duru tano za kwanza, mshindi wa dunia mwaka 2019 Ott Tanak (Estonia) ni baadhi ya madereva wanaopigiwa upatu kushinda mashindano hayo ya kilomita 320.19.

Katika orodha hiyo pia kuna Waingereza Elfyn Evans na Gus Greensmith, Mbelgiji Thierry Neuville, Mhispania Dani Sordo, Mfaransa Adrien Fourmaux, Mswidi Oliver Solberg na Kalle Rovanpera (Finland), Takamoto Katsuta (Japan) na Mwitaliano Lorenzo Bertelli.

Ogier amevuna alama 106 na anaingia Safari Rally na motisha ya kutawala nchini Italia mapema mwezi huu. Anafuatiwa na Evans (95), Neuville (77) na Tanak (49) mtawalia. Macho pia yatakuwa kwa Wakenya Baldev Chager aliyeshinda Safari Rally ilipoandaliwa mara ya mwisho 2019 kama duru ya Afrika na majaribio ya WRC, na mshikilizi wa mataji matano ya Safari Rally Carl Tundo.

Pia, kuna madereva chipukizi McRae Kimathi (26), Hamza Anwar (22) na Jeremy Wahome (22) walioingizwa majuzi kwenye mradi wa Shirikisho la Mbio za Magari Duniani (FIA) kukuzwa kuwa mastaa wa siku za usoni.

Dereva wa pekee mwanamke Maxine Wahome atakuwa wa mwisho kutoka KICC ambako viongozi wakuu wa serikali wanatarajiwa kuhudhuria akiwemo Rais Uhuru Kenyatta. Mkenya pekee hai kuwahi kushinda Safari Rally ilipokuwa kwenye WRC, Ian Duncan (1994) hayuko katika orodha ya washiriki.

  • Tags

You can share this post!

Ubaguzi: Weusi wafaa wajilaumu wenyewe

Vinara wa NASA wawakanganya wafuasi wao