• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 11:29 AM
Ubakaji wakithiri kwa wanawake wakihepa kafyu

Ubakaji wakithiri kwa wanawake wakihepa kafyu

ERIC MATARA na ALICE KARIUKI

WAKENYA wamekuwa wakihatarisha maisha yao wakikwepa vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na Rais Uhuru Kenyatta alipofunga kaunti tano zilizo na maambukizi ya juu ya virusi vya corona.

Visa vya watu kuibiwa mali na kubakwa wakitumia njia za msituni kuingia na kutoka kaunti hizo vimeripotiwa.

Taifa Leo imegundua kwamba maafisa wa serikali katika kaunti za Nakuru na Kericho wanachunguza visa vya ubakaji vilivyoripotiwa na wasafiri waliokuwa wakiingia na kutoka Nakuru.

Waendeshaji wa bodaboda wamekuwa wakiwalenga wasafiri, wanaopitia msituni kukwepa vizuizi vya barabarani, kutekeleza vitendo hivyo na kuwaibia mali yao.

Kisa kimoja kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Londiani, Kaunti ya Kericho mwishoni mwa wiki na mshukiwa mmoja alikamatwa.

Kamanda wa polisi katika Kaunti-ndogo ya Londiani, Bw Rashid Ali alifichua kwamba abiria mmoja alidai kubakwa na mwendeshaji wa bodaboda.

“Mwathiriwa mmoja aliripoti katika kituo cha polisi cha Londiani kwamba alibakwa mwishoni mwa wiki. Mshukiwa huyo alikamatwa na kupelekwa kortini Molo mnamo Jumanne,” alisema Bw Ali.

Taifa Leo ilibaini kwamba abiria huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa akitoka Nairobi kuelekea magharibi mwa Kenya aliposhambuliwa.

Alikuwa amelipa Sh300 kukwepa polisi katika kizuizi cha barabarani kilichoko makutano ya Londiani. Polisi katika kaunti za Nakuru na Kericho sasa wanachunguza uwezekano wa visa kama hivyo katika kaunti hizo.

Inasemekana kuwa katika muda wa siku tatu, wanawake watatu waliripoti kubakwa na waendeshaji wa bodaboda katika kituo cha polisi cha Londiani wakijaribu kuhepa kizuizi cha polisi kwenye barabara ya Mau Summit-Londiani.

Jumatano, kamanda wa polisi katika Kaunti-ndogo ya Molo, Bw Samuel Mukusi pia aliahidi kuchunguza kisa hicho.

“Kufikia sasa, hakuna kisa cha ubakaji kilichoripotiwa katika kituo cha polisi cha Molo lakini tumeacha kuchunguza suala hilo,” alisema.

Mnamo Jumatatu, chifu wa lokesheni ya Tayari, Bw Hassan Waweru, pia alithibitisha kuwa visa vitatu vya ubakaji vimeripotiwa eneo hilo na wasafiri wanaokwepa vizuizi vya barabarani.

“Inasikisha kwamba baadhi ya bodaboda wanawadhulumu wasafiri wanaowavukisha mpaka. Ninahimiza Wakenya kutii maagizo ya serikali, hii ndiyo njia ya pekee ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivi, si adhabu,” alisema Bw Waweru.

Kufikia Jumatano, bodaboda 20 walikuwa wamekamatwa kwa kusaidia wasafiri kukiuka kanuni za kuzuia corona. Kuna hofu kwamba visa vingi vya ubakaji havijaripotiwa, waathiriwa wakiogopa kukamatwa.

“Idadi ya visa vya ubakaji inaweza kuwa ya juu lakini ni wachache wanaoripoti kwa sababu wengi wanaogopa kukamatwa kwa kutumia njia za msituni kukwepa vizuizi vya barabarani. Tunawasaka wanaovitekeleza,” alisema afisa wa polisi katika kizuizi cha makutano ya Londiani.

Haya yanajiri huku afisa mshirikishi wa eneo la Rift Valley, Bw George Natembeya akifichua kuwa maafisa wa polisi katika kaunti za Nakuru na Kajiado wameimarisha usalama katika vizuizi vya barabarani na wanapanga kutumia droni kuwakamata wanaovuka mipaka wakitumia njia za msituni.

You can share this post!

Shirika laonya kuhusu nyama

ARVs: Makanisa yaunga usambazwaji wa haraka