• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ukeketeji Mlima Kenya unavyochochewa na laana

Ukeketeji Mlima Kenya unavyochochewa na laana

Na MWANGI MUIRURI

Changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ukeketaji dhidi ya wanawake wa Mlima Kenya ni laana ya kuachwa na nyanya wengi wa eneo hilo.

Pale ambapo katika uhai wao, nyanya hao wanatoa laana kuwa kila mtoto atakayezaliwa ndani ya familia yake na awe msichana ambaye atapewa jina lake, asiwahi kosa kukeketwa.

“Yaani, nyanya katika familia anasema kuwa jina lake lisiwahi kosa kukeketwa hivyo basi kuweka kizazi chake chote katika utumwa wa kukeketa wasichana,” asema Mwenyekiti wa Muungano wa Maendeleo ya Wanawake (MYWO) eneo hilo Bi Lucy Nyambura (pichani).

Bi Nyambura anaelezea kuwa laana ya mama mzazi katika ukanda wa Mlima Kenya—ambapo jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru huishi kwa wingi—huwa ya kuogofya sana kwa kuwa madhara yake ukiikaidi huwa ni mauti au ulemavu wa kiwango cha juu.

“Laana ya mama mzazi huhangaisha na huwa inasemwa kuwa haina tiba. Ukilaaniwa na mamako, huwa ni sawa na kuhukumiwa kukumbana na mauti. Ni katika hali hiyo ambapo laana hiyo ya ukeketaji ikiachwa, hata iwe familia yenu ni ya wokovu, itabidi sasa muanze kukeketa wasichana wote ambao wako na jina lake,” asema Bi Nyambura.

Anasema kwamba huku juhudi tele za kupambana na ukeketaji wa wanawake zikiwa ndani ya Kaunti za Rift Valley, Mashariki na Kaskazini Mashariki, “uhaini huo bado unaendelezwa katika maeneo ambayo yanadhaniwa kuwa ya kidini na ya ustaarabu wa kijamii,” asema Bi Nyambura.

Naibu Waziri wa Spoti, Utamaduni na Turathi za Kitaifa Bw Zack Kinuthia anasema kuwa uzito wa laana hii ya nyanya kwa watoto wa kike eneo hilo huwa na uzito kwa kuwa “huwa wanaaga dunia kabla ya hawajabatilisha laana hiyo.”

Anasema kuwa mauti ya nyanya hao huwatumbukiza wasichana wa familia hizo katika utiifu kwa laana ya milele hivyo kuwa na ungumu wa kupambana na ukeketaji wa wasichana.

“Utapata kwamba familia imejaa wokovu lakini inaendeleza ukeketaji dhidi ya wasichana. Kuna hata viongozi wa makanisa ambao kwa upande mmoja wanakiri imani ya Mungu lakini kwa upande mwingine wanakiri imani ya miungu ya nyanya walioaga dunia na wakawaachia laana ya kukeketa wasichana wao,” asema Bw Kinuthia.

Katika hali hiyo, Bw Kinuthia anasema ukeketaji katikaMlima Kenya dhidi ya wasichana bado unaendelezwa na kwa kuwa wengi ni wastaarabu ambao sio mila ya dhati ambayo wanatekeleza bali ni kutii laana ya waliokufa na kuoza.

Bi Nyambura anasema kuwa kuna dini ambazo huendeleza Injili za kutii laana za waliokufa hivyo basi kuchochea ukeketaji huo kuendelea.

“Ni katika hali hiyo ambapo utapata baadhi ya wazazi wa eneo hilo wakisaka huduma za ukeketaji hadi katika hospitali za umma na kibinafsi,” akasema Bi Nyambura.

Mshirikishi wa masuala ya kiusalama eneo la Kati mwa nchi Bw Wilfred Nyagwanga alisema kuwa hali hiyo ni ya ukweli na ambapo mikakati ya kupambana na hali hiyo inaendelea.

“Kile sisi katika serikali huwa tunatekeleza sheria wala sio imani na itikadi…Sheria kwa sasa inasema kuwa ni uhaini kukeketa wanawake na huo ndio msimamo wetu,” akasema.

Bw Nyagwanga hata hivyo alikubali kuwa wazazi wengine wakihofia kuandamwa na sheria huwa wanajificha sana wakisaka huduma za wakeketaji hivyo basi kugeuza hali hii yote kuwa ujambazi wa kimyakimya dhidi ya wasichana wadogo.

You can share this post!

Hesabu za Uhuru 2022 zamkosesha usingizi

‘Sauti ya Mnyonge’ anayeendeleza ndoto ya kutetea...