• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Uteuzi wa majaji unatiliwa shaka

TAHARIRI: Uteuzi wa majaji unatiliwa shaka

NA MHARIRI

WIKI hii yote suala kubwa lililo midomoni mwa Wakenya ni jinsi ambavyo Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiichukulia idara ya Mahakama.

Tangu atoe matamshi yake kwenye hotuba ya sikukuu ya Madaraka mjini Kisumu, Rais Kenyatta amekuwa akilaumiwa kuwa anaendelea kudharau mahakama; kwamba anatimiza ahadi yake ya kuiadhibu taasisi hiyo, kutokana na kubatilishwa kwa uchaguzi wa urais mwaka 2017.

Mojawapo ya mambo yaliyomfanya agongane na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga ni kukataa kuwaidhinisha majaji 41 walioteuliwa wakati huo. Kati yao, walikuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa, ambako maelfu ya kesi zimejazana.

Hatimaye jana alifanya uteuzi huo, lakini kukajitokeza mambo mawili. Kwanza, aliwakataa majaji sita, wakiwemo wawili waliohusika kwenye hukumu iliyokataa mswada wa kurekebisha Katiba (BBI).Majaji Joel Ngugi na George Odunga walikataliwa.

Inasemekana wamekataliwa kwa sababu hawajatimiza baadhi ya mahitaji muhimu? Hayo ni mahitaji gani? Je, kuna majaji wangapi kati ya walioteuliwa walio na uprofesa katika masuala ya sheria? Jaji Ngugi ni Profesa na kuteuliwa kwake kuongoza wenzake kuamua kuhusu hatima ya BBI ni ushahidi kuwa wakuu wa idara ya Mahakama wana imani naye.

Jaji Odunga kwa upande wake amekuwa akitoa maauzi yanayoenda kinyume na matakwa ya serikali. Kukataliwa kwa jaji huyo kunaonyesha kwamba lengo halisi la kuteua majaji sasa, ni kuharakisha rufaa ya BBI na kisha iende kwa njia ya kufurahisha wanaoipendekeza.

Lakini kuna uhakika gani kwamba kuongezwa kwa majaji saba wa Mahakama ya Rufaa kutaipa serikali hukumu ya kupendeza?Ukweli utabaki kwamba Rais Kenyatta hakufaa kubadilisha orodha hiyo ya majaji 41 (japo mmoja alifariki dunia).

Kufanya hivyo ni ukiukaji wa Katiba. Ni mfano mbaya kutoka kwa rais wa nchi inayodai kuwa inaheshimu utawala wa sheria.Ni bayana kwamba Rais Kenyatta ameanika mapuuza ya utawala wa sheria.

Ni tabia ambayo inaweza kuigwa na kuendelezwa maafisa wengine wa serikali yake.Kwa kuonyesha upendeleo katika uteuzi huo, uhuru wa mahakama utatiliwa shaka.

  • Tags

You can share this post!

Tanzania kuanza zoezi la utoaji chanjo dhidi ya gonjwa la...

Korti yaagiza wadhifa wa karani wa bunge la Nairobi usalie...