• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Wachimbaji mawe Lamu wataka serikali ipige jeki shughuli zao

Wachimbaji mawe Lamu wataka serikali ipige jeki shughuli zao

Na KALUME KAZUNGU

WACHIMBAJI mawe ya kuchonga na kokoto Kaunti ya Lamu wameilalamikia serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kwa kutelekeza shughuli zao.

Wachimbaji hao kutoka maeneo ya Manda-Maweni, Nairobi Area na Baharini wanasema licha ya kujitahidi kutengeneza mawe mazuri ya kujengea na kokoto, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa imekuwa ikisafirisha vifaa hivyo vya ujenzi kutoka kaunti za nje, ikiwemo Kilifi na Mombasa ili kuendeleza miradi ya ujenzi Lamu.

Zaidi ya wakazi 2000 hutegemea uchimbaji mawe na kokoto ili kukimu familia zao eneo la Manda-Maweni ilhali karibu wakazi 1000 wakitegemea kazi hiyo kujiendeleza maishani kwenye maeneo ya Nairobi Area na Baharini, tarafa ya Mpeketoni.

Wachimbaji mawe eneo la Manda-Maweni, wakiongozwa na Fredrick Otieno. Wanalalama kwamba wametelekezwa na serikali ya kaunti na ile ya kitaifa katika shughuli zao. Picha/ Kalume Kazungu

Msemaji wa wachimba migodi wa Manda-Maweni, Joseph Oduor, alisema hatua ya kaunti na serikali kuu kukosa kutumia vifaa vya ujenzi vinavyotengenezwa Lamu ili kutekeleza miradi mikuu ya ujenzi imepelekea shughuli za wachimba migodi hao kukosa kupanuka.

Alitaja miradi mikuu kama vile ujenzi wa jeti za kisiwa cha Lamu, Mokowe na Mtangawanda, ujenzi wa Bandari ya Lamu (Lapsset) unaoendelezwa eneo la Kililana, ujenzi wa barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen na ujenzi wa makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lam una ile ya kitaifa mjini Mokowe kuwa baadhi ya miradi ambayo vifaa vyake vimesafirishwa kutoka nje ya kaunti ya Lamu.

Bw Oduor alisema endapo kaunti na serikali kuu itabadili nia yake na ianze au iongeze matumizi ya vifaa vya ujenzi vinavyotolewa Lamu, anaamini biashara yao itapanuka na kuwafanya matajiri siku za usoni.

“Tumechoka kutelekezwa katika shughuli zetu. Tunachimba mawe mazuri ya kujengea. Pia tunatengeneza kokoto. Vifaa hivyo ndivyo vimetumika kujenga nyumba na hoteli zote hapa kisiwani Lamu. Inakuaje kaunti na serikali kuu kutumia matofali au kokoto kutoka Kilifi na Mombasa ilhali sisi wenyewe tunatengeneza vifaa hivyo hapa kwetu? Watufikirie sana sisi wenyeji ambao ni wachimba migodi. Tunaumia kwa kukosa soko la vifaa vyetu,” akasema Bw Oduor.

Mchimbaji mawe na kokoto eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni Stephen Kamau, alisema wanalazimika kuuza vifaa hivyo rejareja ili angalau wapate riziki.

Alieleza haja ya serikali ya Kaunti ya Lamu kuwatafutia soko rasmi wachimba mawe hao ili kuwapa motisha kazini.

“Mawe yetu tunauza kwa bei ya rejareja kwa watu binafsi eneo hili. Ingekuwa bora kwa serikali kutupa zabuni za kutengeneza vifaa hivyo kwa miradi yake mikubwa inayoendelezwa hapa Lamu badala ya kusafirisha vifaa kutoka kaunti za mbali,” akasema Bw Kamau.

Naye mtetezi wa haki za raia eneo la Lamu, Francis Mugo, aliwashauri wachimba mawe na migodi kote Lamu waunde muungano utakaowasaidia kupigania haki zao za kimsingi.

“Ni kweli kabisa kwamba tuko na mawe na kokoto nzuri za kujengea zinazotolewa papa hapa kwetu. Ningewashauri wale wote wanaojishughulisha na kazi hiyo hapa Lamu kuunda chama cha ushirika kitakachosaidia kuangazia vilio na pia kupigania haki zao serikalini kwa urahisi,” akasema Bw Mugo.

You can share this post!

ODM wahofia Jubilee inakoroga Raila

Mwanamume apata majeraha kwa kugongwa na gari Thika Road