• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 10:36 AM
Wachungaji wapendekeza adhabu ya kiboko irejeshwe shuleni

Wachungaji wapendekeza adhabu ya kiboko irejeshwe shuleni

Na LAWRENCE ONGARO

WACHUNGAJI wa kidini wa Evangelical and Indigenous Christian Churches of Kenya (FEICCK) kutoka Kiambu na Nairobi, wametoa wito serikali ichukue hatua kali kwa wanafunzi wanaochoma mabweni shuleni.

Wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Glory Outreach Assembly (GOA) wa Kahawa Wendani, Bw David Munyiri, wachungaji hao walipendekeza kuwa serikali iruhusu adhabu ya kiboko shuleni ili wanafunzi waweze kupata funzo kutoka kwa kichapo.

“Tunajua wengi hawatapenda msimamo huo lakini ni sharti amri ya kudumu itekelezwe kwa wanafunzi hao,” alisema Bw Munyiri.

Aliwashauri wazazi wawe mstari wa mbele kuwashauri wana wao kabla ya kupeleka matakwa ya nidhamu kushughulikiwa na mwalimu.

Alieleza kuwa malimbikizo ya ratiba ya masomo, maswala ya ugonjwa wa Covid- 19, na kukaribia kwa mtihani, ni baadhi ya mambo yanayowatia wanafunzi kiwewe, akisema serikali iingilie kati kwa haraka.

Alieleza kuwa kama wachungaji, wanajiandaa kuzuru shule kadha kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu kudumisha nidhamu na kujali maisha yao ya baadaye.

Wachungaji hao walikashifu tabia ya wanasiasa kuwapa vijana kiinua mgongo (hela chache), jambo wanalodai vijana hao hutumia kununua dawa za kulevya na pombe.

Waliwashauri wazazi pia kuwajibika hasa wakati huu wanafunzi wanarejea nyumbani kwa likizo fupi.

“Huu ni wakati wa wazazi hao kuketi chini wa wana wao na kuwashauri kwa kina umuhimu wa masomo na maisha yao ya baadaye,” alifafanua Bw Munyiri.

Walimu pia walishauriwa kufuatilia mienendo kamili ya wanafunzi na hatua kali kuchukuliwa dhidi yao bila kuwadekeza.

Mwenyekiti wa muungano wa FEICCK, Askofu Samuel Ngacha Njiriri, aliwataka viongozi kuwapa mwongozo vijana badala ya kuwapatia pesa kila mara.

“Wanafunzi wengi wanakosa mwongozo maalum kutoka kwa wazazi na hilo ni jambo linalostahili kuchunguzwa kwa makini,” alisema Askofu Njiriri.

Mbunge wa Ruiru Simon King’ara ambaye alihudhuria hafla hiyo katika uzinduzi wa ujenzi wa makao makuu ya Kanisa la GOA, Kahawa Wendani, alisema serikali ina jukumu la kutatua shida hiyo ya wanafunzi.

“Imefika wakati ambapo jambo hilo linafaa kuchunguzwa kwa makini zaidi kwa kufanya utafiti na washika dau wa kielimu ili kupata chanzo cha migomo,” alifafanua mbunge huyo.

Alisema wakati umefika kwa serikali, wazazi, na washika dau wa kielimu kuketi pamoja ili kutanzua chanzo cha migomo ya kila mara.

Alieleza kuwa viongozi pia wasiachwe nyuma katika mjadala huo ili kuwe na mwelekeo mmoja utakaoboresha maswala ya elimu.

You can share this post!

Uhuru aliwapuuza waliotaka nishtakiwe kwa kosa la uhaini...

Aston Villa wamtimua kocha Dean Smith kwa sababu ya matokeo...

T L