• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wahisani waombwa kujitokeza kusaidia shule ya watoto viziwi Mwingi

Wahisani waombwa kujitokeza kusaidia shule ya watoto viziwi Mwingi

Na BONIFACE KANYALI 

Wahadhiri na wanafunzi wa chuo kikuu Cha South Eastern University of Kenya (SEKU), Alhamisi Oktoba 5, 2023 walitoa msaada wa vyakula na nguo kwa wanafunzi wa shule ya watoto walio na ulemavu wa kusikia mjini Mwingi.

Wakiongozwa na Dkt Sara Ngesu anayesimamia kitengo cha Huduma kwa Jamii na masuala ya Ulemavu, wanafunzi na wahadhiri walizuru shule hiyo na kulakiwa kwa mbwembwe na vifijo.

Akizungumza baada ya kutoa msaada wao, Bi Sara Ngesu alisema kuwa zoezi hili liliwezeshwa kutokana na ukarimu wa wahadhiri na wanafunzi wa SEKU waliochangia kifedha na misaada ya nguo kama njia moja ya kuendeleza ubinadamu kwa watoto hao wasiojiweza.

“Tumewezeshwa kuja hapa leo kufuatia kujitolea kwa wahadhiri na wanafunzi wa shule yetu kwa hali na mali, ili kuwafanya wanafunzi katika shule hii kujihisi kama binadamu wengine wenye uwezo wa kusikia,” alieleza Dkt Ngesu.

Ngesu alieleza kuwa shule hii ya watoto wenye ulemavu wa kusikia ya Mwingi iko na changamoto chungu nzima, kutoka upungufu wa chakula, malazi na vyoo ambavyo vinahitajika kwa dharura shuleni humo.

“Ukiangalia vyoo vyao viko karibu kujaa, changamoto za chakula na malazi pia zinawakodolea macho wanafunzi wa shule hii. Mara kwa mara, walimu wa shule hii hulazimika kutumia fedha zao kuwasaidia wanafunzi hawa kwani wengine ni wachanga mno,” aliongeza Bi Ngesu.

Mhadhiri huyu aliwataka wahisani wengine kujitolea na kusaidia shule hii, ili kuboresha maisha ya wanafunzi wnaoishi humo.

Usimamizi wa shule hii na wanafunzi walionyesha furaha kuu kutokana na msaada waliopokea kutoka SEKU.

 

Wanafunzi na wahadhiri wa Chuo kikuu cha SEKU, Kitui walipotembelea shule ya watoto walio na ulemavu wa kusikia ya Mwingi, Kaunti ya Kitui. Picha|Boniface Kanyali
  • Tags

You can share this post!

Daktari athibitisha mwanamume aliyefariki baada ya kunywa...

Polisi wamsaka mwanamume anayedaiwa kumuua mke, mtoto...

T L