• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wahubiri wakemea sheria ya kutoza maombi ushuru

Wahubiri wakemea sheria ya kutoza maombi ushuru

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADHI ya wahubiri na makasisi mjini Kisii wamekerwa na mipango ya serikali ya kaunti hiyo kutoza ushuru makanisa yanayofanya maombi ya usiku, maarufu kama kesha.

Mswada wa Fedha ambao tayari umepitishwa na Bunge la Kaunti, unapendekeza makanisa yanayotaka kuendesha kesha, yalipe Sh5,000 kila wiki, mara tu Gavana Simba Arati atakapoutia saini.

Mhubiri yeyote atakayeingia mitaani kueneza Injili atalazimika kutenga Sh2,000 kwa wiki ili aruhusiwe kuhubiri.

Wahubiri wanaotumia magari ya kubebea mizigo yenye vipaza sauti watalipa hadi Sh20,000 kwa wiki.

Siku chache baada ya mswada huo kupitishwa, baadhi ya makasisi wamekashifu uongozi wa Kaunti kwa kuanzisha ada hizo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wachungaji na Makasisi wa Kisii, Lawrence Nyanuga, ametaja uamuzi huo kuwa wa kusikitisha.

“Wakati wa kampeni walikuwa wakituomba tuwaombee na kuwataka wanachama wetu kuwaunga mkono. Sasa wametugeuka na wanataka kututoza ushuru,” akasema.

Alisikitika kuwa makanisa yanatozwa kodi badala kuungwa mkono na serikali ili yawezeshwe kufikia nyoyo za watu wengi kwa njia ya uinjilisti.

“Katika hali nyingi, kesha hazivutii watu wengi. Serikali ya kaunti inafikiri kwamba tunapata pesa kwa kufanya kesha za usiku lakini sivyo. Makanisa si mashirika ya kutengeneza faida na kwa hivyo hayafai kuchukuliwa vinginevyo,” alisema kasisi Nyanuga.

Huku makasisi hao wakishikilia kuwa kutoza ushuru makanisa ni sawa na kumtoza Mungu ushuru, wakazi wengine wa Kisii wamefurahia hatua ya makanisa kulipa ushuru huo wakisema kuwa, itasaidia kudhibiti wahubiri na makanisa yayocheza muziki kwa sauti ya juu haswa katika maeneo ya makazi.

“Nimefurahi. Huwa sipati hata lepe la usingizi siku za Ijumaa katika eneo ninaloishi. Sauti zinashindana kutoka kwa makanisa mbalimbali yaliyo hapo,” akasema mkazi wa Daraja Mbili, Bw Enock Ogoti.

“Ninaipongeza Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa pendekezo hilo ambalo kwa maoni yangu, lilipaswa kuletwa mapema. Hili likishaanza kutekelezwa, nina hakika litapunguza makanisa na maeneo mengine ya ibada kupiga muziki kwa sauti ya juu,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Daktari abaini wanafunzi wa Amabuko waliugua kwa kula...

Kabura kujitetea katika kesi ya uporaji wa Sh791 milioni za...

T L