• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Wahudumu wa afya wanunuliwa pikipiki kulinda wakazi dhidi ya corona

Wahudumu wa afya wanunuliwa pikipiki kulinda wakazi dhidi ya corona

Na WACHIRA MWANGI

KAUNTI ya Mombasa imenunua pikipiki mbili kwa kila kaunti ndogo, ili kuwawezesha wahudumu wa afya kuendesha juhudi za kukabiliana na visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo pia inalenga kurahisisha juhudi za kukusanya sampuli za kufanyiwa utafiti kuhusu virusi, usambazaji wa vifaa vya kutoa chanjo kati ya shughuli zingine.

Akihutubu wakati wa utoaji wa pikipiki hizo, Afisa Mkuu wa Afya katika kaunti hiyo Bi Pauline Odinga alisema, hilo litawawezesha wahudumu kufika katika maeneo ya ndani ambayo ni vigumu kuyafikia kwa magari.

“Tulinunua pikipiki nane kwa kutumia fedha za kukabiliana na janga la virusi vya corona. Tulifanya hivyo kutokana na matatizo yaliyoibuka kwenye juhudi zetu kuyafikia maeneo ya ndani,” akasema Bi Oginga.

Alisema pikipiki hizo ni zenye muundo maalum, hivyo zinaweza kutumika kwenye shughuli zingine kama utoaji chanjo, ukusanyaji sampuli na kusafirisha vifaa mbalimbali vinavyohitajika nyanjani.

Alisema kaunti hiyo ina maeneo ambako magari hayawezi kufika kwa urahisi.

“Kwa sasa, tunaweza kuyafikia hayo ili kutoa huduma bora kwa wananchi. Hili pia litapunguza visingizio ambavyo vimekuwa vikitolewa na baadhi ya wafanyakazi kwa kutotimiza malengo yao ya kikazi,” akaongeza.

Alieleza kuwa kaunti pia imeimarisha juhudi kwenye mpango wa kuhakikisha afya bora miongoni mwa wanafunzi shuleni. Hilo ni kupitia ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya (KRCS) na wahudumu wa afya wa kujitolea.

Bi Oginga alisema kaunti hiyo bado ina visa vya maambukizi, hivyo wakazi wanapaswa kuendelea kuzingatia masharti ya kudhibiti virusi hivyo kuenea.

You can share this post!

Macho yote kwa Haji kuhusu wizi wa mabilioni Kemsa

ODM pia ilaumiwe kwa uzembe wa serikali – Ruto