• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Maji yamkaribia Trump shingoni mshirika wake wa pili akikiri kujaribu kubatilisha kura ya urais ili kumfaidi

Maji yamkaribia Trump shingoni mshirika wake wa pili akikiri kujaribu kubatilisha kura ya urais ili kumfaidi

LABAAN SHABAAN na MASHIRIKA

WAKILI Sidney Powell amekiri alikula njama ya kupindua matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Georgia kwa mapendeleo ya Rais wa Amerika wakati huo Donald Trump.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2020, Powell alikuwa wakili wa Trump.

Mnamo Alhamisi, Oktoba 19, 2023 mwanasheria huyo alihukumiwa kifungo cha nje cha miaka sita na kutakiwa kulipa faini ya $6, 000 (Sh899, 280).

Pia, atagharamika fidia ya $2, 700 (Sh404,676) kwa Ofisi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni Georgia.

Vile vile, wakili huyu amehitajika kuandika barua ya msamaha kwa wananchi wa Georgia.

Powell alifaa kufika kortini Jumatatu na mshukiwa mwenzake Kenneth Chesebro.

Sasa, Chesebro atasimama kizimbani pekee yake juma lijalo.

Ripoti ya uchunguzi wa kamati ya bunge ilimtaja Chesebro kuwa mkarabati wa uchaguzi bandia.

Bunge limemhusisha na njama ya udanganyifu jimboni Georgia na majimbo mengine angalau sita nchini Amerika.

Powell atatoa ushahidi dhidi ya washukiwa wenzake na hatakubaliwa kuonana na mashahidi ama washukiwa wengine.

Chesebro alikataa mpango sawia na Powell uliotolewa na Ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Kaunti ya Fulton.

Angekubali, Chesebro angelazimika kutoa ushahidi dhidi ya washukiwa wenzake akiwemo Donald Trump.

Kadhalika, angetakiwa kuomba msamaha kwa wananchi wa Georgia na kupewa kifungo cha nje cha miaka mitatu pamoja na kutozwa faini ya $10, 000 (Sh1, 498, 800)

Powell na Chesebro ni miongoni mwa jumla ya washukiwa 19, pamoja na Donald Trump, wanaokabiliwa na mashtaka ya kupindua uchaguzi wa urais wa 2020 wa Jimbo la Georgia.

Trump amepinga mashtaka dhidi yake katika kesi ya Georgia.

Kwa ujumla, rais huyo wa zamani anakabiliwa na tuhuma 13 – ikiwemo ya ufisadi – kwa madai ya kushinikiza maafisa wa uchaguzi kubadilisha matokeo ya kura ya urais.

Trump amepinga mashtaka dhidi yake akisema kesi hii imesukumwa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Demu aliwahi kuniambia anapenda ufyekaji mzuri, sasa anadai...

Wakazi wa Liwale, Tanzania wadai uhaba wa maji unahatarisha...

T L