• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wakazi wataka Rais aepuke siasa za urithi

Wakazi wataka Rais aepuke siasa za urithi

Na KNA

WAKAZI wa Nyeri, sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kujishughulisha na jinsi Wakenya watakavyomkumbuka baada ya kustaafu badala ya kutumia nguvu na muda aliosalia nao afisini katika kupanga siasa za urithi.

Wakazi hao hasa walitofautiana na mkutano ambao Rais aliripotiwa kushiriki na vinara wa upinzani katika ikulu ya Mombasa, waliodai ulilenga kuwatenga baadhi ya wanaopanga kumrithi katika uchaguzi mkuu ujao.

Rais Kenyatta aliwakutanisha viongozi wa One Kenya Alliance (OKA), ODM, ANC na Ford Kenya kwa lengo la kuwashawishi kumuunga mkono mgombea mmoja atakayemenyana na Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Hata hivyo, wakazi hao wanamtaka Rais aelekeze nguvu zake katika kusuluhisha changamoto mbalimbali zinazokabili kaunti hiyo na kuwaacha waamue wenyewe ni nani watakayempigia kura kuwa rais katika uchaguzi mkuu ujao.

Walihoji kuwa Rais ana mambo mengi ya kushughulikia ikiwemo kuimarisha uchumi unaoyumbayumba, janga la Covid-19 na kuhakikisha amani inadumishwa taifa likielekea kwenye uchaguzi.

“Muhimu ni iwapo Rais ataimarisha uchumi, anawasaidia vijana kwa kuunda nafasi za kazi na kuhakikisha Wakenya wote wanapatiwa chanjo dhidi ya Covid-19. Uamuzi kuhusu ni nani atakayekuwa Rais mpya utatolewa nasi wapiga kura,” alisema Bi Cecilia Wandeto, mkazi wa Nyeri akizungumza na KNA.

You can share this post!

Lewandowski aweka rekodi ya ufungaji katika mechi za...

Mpiganiaji demokrasia Nthenge azikwa kwake bila mbwembwe