• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wakenya milioni 1.4 wanakabiliwana baa la njaa – Ripoti

Wakenya milioni 1.4 wanakabiliwana baa la njaa – Ripoti

Na STELLA CHERONO

WATU milioni 1.4 wanakabiliwa na baa la njaa nchini Kenya, idadi ambayo ni maradufu ya idadi iliyoripotiwa mnamo 2020, ripoti ya serikali na Umoja wa Mataifa (UN) imeonya.

Uchunguzi wa hali ya uwepo wa chakula nchini ulioendeshwa na Makundi ya Kusimamia Hali ya Chakula Nchini na UN, imebaini kuwa angalau watu 288,000 kutoka kaunti nane nchini wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.

Kaunti hizo ni Mandera, Wajir, Garissa, Tana River, Marsabit, Samburu, Turkana na Isiolo.Ripoti iliyoandaliwa baada ya ukaguzi huo pia inasema hali hiyo imechangiwa na janga la Covid-19, magonjwa ya mifugo, uvamizi wa nzige na mapigano na utovu wa usalama. Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula.

“Kudhibitiwa kwa uagizaji wa chakula kutoka nje kumechangia uhaba wa vyakula vya kupambana na athari zinazohusiana na Covid-19 na lishe bora kwa watu kutoka familia maskini na watoto ambao hawajatimu miaka mitano,” ripoti hiyo iliyotathimini hali wakati wa mvua fupi ikasema.

Ripoti hiyo inakadiria athari ya uvamizi wa nzige kuwa uharibifu wa zaidi ya hekta 310 za mashamba yenye mimea ya chakula ambayo ni sawa na asimilia 65 maeneo yote yenye mashamba.

Wadudu hao pia waliharibu zaidi ya hekta 7,500 ya maeneo ya lishe ya mifugo.

“Katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa kaunti za Turkana, Samburu na Marsabit, nzige pia wameharibu sehemu kubwa ya maeneo ya kulishia mifugo kwani wamekuwa wakila nyasi na matawi ya miti.

“Kulikuwa na visa vya mifugo kuhara na hata kufa baada ya kula kinyesi cha nzige hao ambayo pia kimeathiri vyanzo vya maji. Uchafu kutoka nzige hao pia umegunduliwa kusababisha magonjwa ya tumbo kwa binadamu,” ripoti hiyo inasema.

Pia inasema kuwa mizozo kati ya binadamu na mifugo na mapigano ya kikabila pia yanachangia ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji chakula cha msaada.

“Mapigano ya kung’ang’ania lishe na maji pia yamechangia ongezeko la mapigano kati ya jamii zinazoishi katika maeneo yanayokumbwa na uhaba wa rasilimali hizo,” ripoti hiyo inaongeza.

Uzalishaji wa maziwa, ripoti hiyo inasema, pia umepungua kutokana na uhaba wa lishe hali inayochangia mifugo kutembea kwa hatua ndefu.Kaunti za Turkana, Wajir, Mandera, Garissa, Marsabit na Samburu ndizo zimeorodheshwa kama zile ambazo zinaendelea kukabiliana na baa la njaa.

Kaunti zinazokabiliwa na utapia mlo; Garissa, Wajir, Mandera,Isiolo, Samburu, Turkana, maeneo bunge ya Horr Kaskazini na Laisamis katika kaunti ya Marsabit na Tiaty katika kaunti ya Baringo.

“Kwa jumla, watoto 541,662 wenye umri wa kati ya miezi sita na 59 na akina mama wajawazito 98,759 na wanaonyonyesha wanahitaji kutibiwa utapia mlo,” ripoti hiyo inaeleza.

You can share this post!

Mutua Katuku aondolewa kwenye uwaniaji useneta Machakos

BIG 3 COAST LADIES TOURNAMENT: MTG United yajiondoa dimba...