• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wakenya wamtarajia Rais kuangazia shida zao akituhubia Bunge Alhamisi

Wakenya wamtarajia Rais kuangazia shida zao akituhubia Bunge Alhamisi

ROSELYNE OBALA na SAMWEL OWINO

WAKENYA wanasubiri kwa hamu kuona iwapo Rais William Ruto ataangazia changamoto nyingi zinazowaathiri anapotoa hotuba yake ya kwanza bungeni kuhusu rekodi ya utendakazi wa serikali yake.

Hotuba ya Rais kuhusu Hali ya Kitaifa inajiri wakati Wakenya wanazongwa na kupanda kwa gharama ya maisha serikali ikionya kuwa, huenda bei ya petroli ikapanda hadi Sh300 kwa lita.

Dkt Ruto anatarajiwa kuwaelezea Wabunge na maseneta jinsi serikali yake imetekeleza sera yake ya kiuchumi maarufu kama “Bottom Up” ndani ya mwaka mmoja baada ya kuchukua usukani.

Kulingana na kipengele cha 132 cha Katiba Rais anatarajiwa kuripoti bungeni kuhusu hatua ambazo serikali yake imepiga katika utekelezaji Maadili ya Kitaifa, utekelezaji wa majukumu yake ya kimataifa na utumishaji wa usalama wa kitaifa.

Mbunge Maalum John Mbadi anasema Rais Ruto hana jingine ila kuangazia masuala yenye umuhimu kwa Wakenya kama vile gharama ya maisha na bei ya mafuta.

“Amekuwa akitutoza ushuru wa juu na sasa sharti aelezee nchini kazi ambayo pesa hizo za ushuru zimefanya,” akasema. “Sharti aeleze mikakati ambayo ameweka kufufua uchumi kwa sababu sidhani kama kuna Wakenya ambao wanayo matumaini kuwa ataboresha uchumi wa nchini. Sharti azingatie ukweli anapozungumzia masuala haya kwa sababu wadhifa anaoushikia haumruhusu kudangaya,” Bw Mbadi akaongeza.

Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia alisema anamtarajia Rais kufafanua jinsi atashughulikia suala la mzigo mkubwa wa madeni, ukusanyaji wa ushuru na namna ambavyo pesa zilipatikana zimetumika kulipa madeni.

“Vile vile, ningemtaka Rais Ruto kuangazia mfumo mpya wa ufadhiliwa wa masomo ya vyuo vikuu kwa sababu ni wazi kuwa baadhi ya wazazi na wadau wengine hawauelewi,” akasema mbunge huyo anayehudumu muhula wa kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Avunja mbavu waumini kuomba pasta idhini ili aoe mke wa pili

Mwanadada kila akilala anaota jinsi ‘ex’...

T L