• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
Wakfu wa Jungle Foundation watoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wanafunzi Kiambu

Wakfu wa Jungle Foundation watoa mafunzo ya huduma ya kwanza kwa wanafunzi Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

WAKFU wa Jungle Foundation umejitolea kuhamasisha wanafunzi katika shule za msingi kuhusu utoaji wa huduma ya kwanza (First Aid) wakati wa ajali.

Afisa wa kusimamia shughuli hiyo Bi Joyce Njeri, anaeleza kuwa wasimamizi wa wakfu huo kwa muda wa wiki kadha wamezunguka katika kaunti nzima ya Kiambu wakiwahamasisha walimu na wanafunzi wa shule za msingi jinsi ya kutoa usaidizi wa dharura kunapotokea ajali wakati wowote.

“Tuliona ya kwamba ni vyema kuwapa wanafunzi mwongozo jinsi ya kusaidia mtu yeyote wakati panapotokea ajali, iwe nyumbani ama mahali popote pale,” alisema afisa huyo.

Alisema mpango huo umepokelewa vyema na wazazi wa wanafunzi hao wakisema ni njia mojawapo ya kuwapa wanafunzi ujuzi wa kujitegemea wakati wa “shida ya ghafla”.

Mnamo Alhamisi wakfu huo ulizuru shule kadha katika Kaunti ya Kiambu.

Alitaja baadhi ya ajali hizo kuwa ni zile za vyombo vya usafiri, mikasa ya moto, na  nyingine zinazohitaji huduma ya kwanza.

Baadhi ya shule walizozuru ni ile ya msingi ya Kianjau mjini Thika, ile ya Gatuura mjini Limuru na ya Ndula iliyoko Thika Mashariki.

Wanafunzi wafuatilia maelezo kuhusu huduma ya kwanza yaani First Aid. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati wa ziara hiyo, wanafunzi walipewa hamasisho kuhusu maambukizi ya Covid-19 na jinsi wanavyostahili kukabiliana na janga hilo.

Wakati huo pia wanafunzi hao walipokea barakao, na sanitaiza huku kila mmoja akishauriwa kuzingatia sheria na kanuni za kuzuia kuenea kwa Covid-19.

Wakfu wa Jungle Foundation unapanga kuzuru shule zote katika Kaunti ya Kiambu ili kuona ya kwamba unawahamasisha wanafunzi wote kwa manufaa yao wenyewe.

Bi Njeri alitoa wito kwa kila mmoja popote alipo ajitahidi kupata ujuzi kiasi kuhusu huduma ya kwanza.

Alisema mara nyingi ajali inapotokea watu wengi hubabaika wasijue la kufanya na kwa hivyo “kuwa na ujuzi kidogo ni muhimu kwa kila mmoja wetu.”

You can share this post!

UMBEA: Je, wewe ni gusa mara moja au mbio ndefu na hufiki...

Crystal Palace yapiga Spurs breki kali katika EPL