• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Wakulima waanza kugeukia mitambo ya jadi kuepuka gharama ya petroli, umeme

Wakulima waanza kugeukia mitambo ya jadi kuepuka gharama ya petroli, umeme

NA RICHARD MAOSI

MATUMIZI ya zana za kitambo kusaga mahindi au kukoboa mpunga yameanza kufikiriwa upya na wakulima wadogo mashinani ili kuwasaidia kuimarisha shughuli ya usindikaji wa mazao ghafi.

Hii ni kutokana na mfumuko wa bei ya mafuta ya petroli jambo linalofanya gharama ya uzalishaji kupanda.

Mojawapo ya mashine hizi ni mtambo wa usagaji – grinder ambao hautumii dizeli wala stima ila unamhitaji mkulima kutumia nguvu kazi za kibinadamu wakati wa kukoboa mazao.

Katika eneo la Bureti Kaunti ya Kericho, tunakumbana na Kennedy Cheruiyot ambaye anatufichulia manufaa ya mtambo wa grinder ambao miaka ya awali ulikuwa ukiwasaidia wakulima kusindika nafaka.

Anasema mtambo wenyewe ulitumika msimu wa kiangazi wakati ambao wakulima wengi walikuwa wamevuna mahindi yao na kuyakausha.

Kinyume na mitambo ya kisasa ambayo huendeshwa kwa kutumia petroli au stima, mtambo huu wa jadi, ulikuwa ukizungushwa na mkulima wakati wa kuongezea nafaka thamani.

Kwa upande mwingine Millicent Obonyo mtaalam wa kilimo asilia, anasema kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta, bei ya nafaka kama vile mahindi itaendelea kupanda.

Hivyo basi, anawahimiza wafanyibiashara wa mahindi kukuza chakula mbadala chenye virutubishi sawia na mahindi.

Aidha anawahimiza kutumia mitambo ya kiasili kama grinder kuongezea mahindi yao thamani ili yaweze kudumu kwa muda mrefu kwa ajili ya matumizi ya baadye.

Hata hivyo, kwa sababu ya gharama ya juu ya mafuta, baadhi ya wakulima mashinani wameanza kuwazia kurudia manufaa ya mtambo wenyewe ambao kwa njia moja utawasaidia kujiongezea faida.

Aidha matumizi yake ni mepesi wala hauchafui mazingira kwa kufuka moshi mwingi ikilinganishwa na mitambo ambayo imezoeleka.

Gharama

Gharama huwafanya baadhi yao kuuza mazao mapema ili kuepuka gharama ya usindikaji ambayo huja na mahitaji mengi ya umeme au mafuta.

Kwa upande mwingine, bei ghali ya mafuta imewafanya wakulima kutumia hela nyingi kusafirisha mazao yao kutoka shambani mpaka sokoni.

Jambo ambalo limefanya baadhi ya wanunuzi kutafuta mazao hadi kwenye mashamba ya wakulima kwa gharama yao wenyewe.

Matumizi ya Grinder

Kuna aina mbili ya mitambo ya grinder mojawapo ukiwa umeundwa kwa mbao na nyingine kwa chuma dhabiti.

Mitambo yenyewe ilitumika kulingana na majira ambapo grinder ya mbao ilitumika msimu wa mvua na ile ya chuma ilitumika msimu wa kiangazi.

Cheruiyot anasema grinder ya mbao, iliendeshwa kwa kasi ya maji huku ya chuma ikiendeshwa kwa mkono na binadamu.

“Ni mtambo wa kukoboa mahindi na manufaa yake ni kwamba hudumisha virutubishi vyote vya mazao.

Ingawa huchukua muda mrefu kusindika aina mbalimbali ya nafaka za mkulima, gharama ya uzalishaji ni nafuu kwani mtambo wenyewe hautegemei petroli,” anaeleza Cheruiyot.

Anaongeza, “Ni mtambo ambao unafaa sana kwa matumizi ya nyumbani hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na stima.

Pia unaweza kutumika kibiashara kwa ajili ya kutengeneza aina mbalimbali ya unga kutokana na nafaka mbalimbali.”

  • Tags

You can share this post!

Hasara mvua ikiendelea kuponda nchi

Avunja mbavu waumini kuomba pasta idhini ili aoe mke wa pili

T L