• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Hasara mvua ikiendelea kuponda nchi

Hasara mvua ikiendelea kuponda nchi

WAANDISHI WETU na KNA

Mvua kubwa inayonyesha maeneo mengi nchini imesababisha hasara mafuriko yakitatiza wakazi huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ikisema inatarajiwa kuendelea hadi Januari mwaka ujao.

Maelfu ya watu wametoroka makwao, barabara kuharibiwa na huduma za stima kukatizwa.

Katika kaunti ya Homa Bay wakazi 500 wa eneo la Karachuonyo waliachwa bila makao baada ya nyumba zao kuathiriwa na mafuriko.

Watu hao wanatoka kata za Kamser Nyakongo, Central Karachuonyo na Kogweno Oriang’. Kwa sasa waathiriwa wamepiga kambi katika shule ya msingi ya Yala na zahanati ya Kogembo.

Gavana Gladys Wanga alisema kwamba serikali yake imeweka mikakati ya kuhakikisha familia zilizoathiriwa zinapata misaada.

Katika kaunti ya Isiolo familia zaidi ya 1000 zinahitaji misaada kwa dharura baada ya nyumba zao kufurika maji.

Katika kaunti ya Nyeri, mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi katika vijiji vya Kagongo , Kamakwa, wadi ya Mukaro, Nyeri ya Kati.

Afisa Mkuu wa Masuala ya Jamii katika serikali ya kaunti ya Nyeri Joe Ngethi alihakikishia wakazi watapata msaada.

Katika kaunti ya Garissa mvua kubwa inayonyesha eneo hilo ilikatiza shughuli za uchukuzi katika kaunti ndogo ya Ijara.

Mvua iliyonyesha kwa siku tatu pia imekatiza umeme katika mji wa Masalani.

Wakazi wamemtaka Gavana wa kaunti jirani ya Tana River Bw Dhadho Godana na mwenzake wa Garissa Bw Nadhif Jama kuwasaidia kutengeneza daraja ambalo limesombwa na mvua na kuwafanya wakazi wa kaunti hizo mbili kutatizika kusafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine.

Kulingana na mwenyekiti wa jamii ya Masalani Bw Abdullahi Abdi na aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Kaunti ya Ijara Bw Mohamed Gure na Ubah Yasin, na Ruth Kimani ambao ni wachuuzi wa mboga katika mji wa Masalani kuna haja ya kutenga fedha za ujenzi wa barabara ya kilomita 18 inayounganisha Masalani na Tana River.

Mnamo Jumatatu, Idara ya Utabiri wa Hewa ilisema kuwa mvua ya msimu huu itakuwa kubwa na katika baadhi ya maeneo itaendelea hadi Januari 2024.

Maelfu ya wenyeji wanaopakana na Ziwa Baringo wanaishi kwa hofu ya mafuriko kufuatia mvua kubwa inayonyesha eneo hilo.

Wakazi hao wana wasiwasi kwamba iwapo mvua kubwa itaendelea kunyesha, huenda maji katika Ziwa hilo yakaongezeka na kusababisha mafuriko katika baadhi ya vijiji vinavyopakana na Ziwa hilo.

Miongoni mwa vijiji hivyo ni Leswa, Loruk, Noosukro, Kokwa Island, Kampi Samaki, Sokotei, Lorok, Kiserian, Ruggus, Loitip, Mukutani Ndogo, Ng’ambo, Sintaan, Salabani, Ilng’arua, na Longeiwan.

Fox Oduor, mwelekezi wa watalii katika Ziwa hilo, alidokeza kuwa tangu mvua kubwa ianze kunyesha mwezi mmoja uliopita, viwango vya maji katika Ziwa hilo vimeongezeka kwa karibu na mita.

“Hii ni dalili kwamba iwapo mvua itaendelea kunyesha, tunaweza kukabiliwa na mafuriko tena. Kulingana na vile tuliona hapo awali, Ziwa hilo huongezeka polepole kabla ya kuvunja kingo zake, na kuzamisha miundo iliyo karibu,” akasema Bw Oduor.

Ripoti ya Florah Koech, George Odiwuor na KNA

  • Tags

You can share this post!

Matumaini teknolojia mpya ya kutibu ugonjwa wa selimundu...

Wakulima waanza kugeukia mitambo ya jadi kuepuka gharama ya...

T L