• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wakulima wakesha ndani ya mashamba wezi wakivizia mazao

Wakulima wakesha ndani ya mashamba wezi wakivizia mazao

NA RICHARD MAOSI

MSIMU wa kuvuna unapokaribia, wakulima wa mahindi na ndizi kutoka Kinangop na Limuru wamesema wanalazimika kukesha ndani ya mashamba yao wakilinda mazao yao yasiibwe.

“Hivi sasa mahindi na ndizi ni kama dhahabu,” amesema Bw Tom Ngugi, ambaye ni mkazi wa eneo la Kamangu katika Kaunti ya Kiambu.

Bw Ngugi ameambia Taifa Leo kwamba alikuwa na migomba 12 ya ndizi lakini hivi sasa amebakisha mitatu tu baada ya wezi kuiba.

Amesema kwamba bei za mbegu na pembejeo za kilimo zimekuwa ghali mno na kwa sasa bei ya kilo 90 za mahindi ni kati ya Sh5,600 na Sh6,000.

Naye Bw Gabriel Gicharu kutoka eneo la Kimende, anasema amekuwa akikuza mahindi tangu mwaka wa 2018. Alitarajia kuvuna magunia 18 kutoka katika kipande cha ardhi cha ekari moja ila alipata mifuko saba tu baada ya wezi kuvuna sehemu kubwa katikati ya shamba..

“Nilishtuka usingizini lakini nilipojaribu kuwafukuza walipotelea gizani kwa kutumia pikipiki,” anasema.

Kwa upande mwingine, Bw Gicharu anasema ingawa mahindi yake yamekomaa, hana njia ya kuyakausha kwa sababu mvua ya El Nino imeanza kushuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi.

“Nikivuna mahindi yakiwa yangali mabichi inamaanisha nitakuwa na kazi nyingi ya kuyakausha. Inanilazimu kukesha ndani ya shamba kwa siku kadhaa,” akasema.

Na sio hilo tu anasema amekuwa akikuza mahindi ili apate majani ya kulisha mifugo yake, haswa ng’ombe wa maziwa, lakini hivi sasa wezi wanalenga mahindi pamoja na majani.

Hii ni baada ya gharama ya lishe ya mifugo kupanda kupita kiasi ndiposa akajifunza jinsi ya kutengeneza ‘silage’.

Anashangazwa kuwaona wezi wakifagia kila kitu shambani bila kusaza makapi ya mahindi, hii ikimaanisha huwa wamepata soko la majani kwa wakulima wa ng’ombe wa maziwa.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza wamepoteza dira, asema Raila

Shujaa yajikatia tiketi ya robo-fainali Kombe la Afrika

T L