• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Shujaa yajikatia tiketi ya robo-fainali Kombe la Afrika

Shujaa yajikatia tiketi ya robo-fainali Kombe la Afrika

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Shujaa imetinga robo-fainali ya Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande baada ya kulipua Namibia kwa pointi 50-0 na Nigeria 34-10 katika Kundi B jijini Harare, Zimbabwe, Jumamosi.

Vijana wa kocha Kevin ‘Bling’ Wambua, ambao watafunga siku dhidi ya Zambia saa kumi na dakika 34 jioni, walifungua kampeni kwa kuzamisha Nigeria kupitia miguso ya Nigel Amaitsa (mitatu), nahodha Vincent Onyala (miwili) Festus ‘Smardi’ Shiasi (mguso mmoja) pamoja na mikwaju miwili kutoka kwa nahodha Anthony Omondi.

Samuel ‘TinTin’ Asati alichangia pakubwa katika mchezo wa Kenya ikiwemo pasi za mwisho zilizozalisha mguso mmoja wa Onyala na mwingine wa Amaitsa.

Fredrick Henry-Ajudua alifungia Nigeria miguso yake miwili bila mikwaju baada ya kufuatuka na kuacha Wakenya hoi.

Katika mechi ya pili, Kenya ilionekana kuimarika zaidi ilipofikisha alama 50 bila jibu. Ilipata miguso kutoka kwa Patrick Odongo, Onyala na John Okoth (miwili kila mmoja) na Wekesa na Ooro (mguso mmoja kila mmoja) na mikwaju mitano kutoka kwa Omondi.

Mshindi wa dimba hilo la mataifa 12 ataingia Olimpiki 2024 moja kwa moja, huku nambari mbili na tatu wakishiriki mashindano ya mwisho ya dunia ili kupata tiketi.

Asati (KCB), (Strathmore Leos), William Mwanji (Kabras Sugar), Beldad Ogeta (Menengai Oilers), Patrick Odongo (Daystar Falcons) na Festus Shiasi (KCB) wanachezea Shujaa kwa mara ya kwanza kabisa.

Makundi:

Kundi A: Afrika Kusini, Madagascar, Tunisia, Cote d’Ivoire

Kundi B: Kenya, Zambia, Namibia, Nigeria

Kundi C: Uganda, Zimbabwe, Burkina Faso, Algeria

Ratiba na matokeo (Septemba 16):

Zimbabwe 12 Burkina Faso 12, Uganda 45 Algeria 7, Zambia 31 Namibia 12, Kenya 34 Nigeria 10, Madagascar 43 Tunisia 5, Afrika Kusini 39  Cote d’Ivoire 0, Zimbabwe v Algeria, Uganda v Burkina Faso, Zambia 38 Nigeria 12, Kenya 50 Namibia 0, Madagascar 40  Cote d’Ivoire 5, Afrika Kusini v Tunisia, Burkina Faso v Algeria, Namibia v Nigeria, Kenya v Zambia (4.34pm), Tunisia v  Cote d’Ivoire, Afrika Kusini v Madagascar, Uganda v Zimbabwe.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wakesha ndani ya mashamba wezi wakivizia mazao

Mchakato wa kumtimua Nyaribo waanza mzozo ukichacha

T L