• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Walalamikia kelele za maeneo ya burudani katika mitaa ya makazi

Walalamikia kelele za maeneo ya burudani katika mitaa ya makazi

NA SIAGO CECE

WAKAZI wa Diani wamelalamikia kelele kutoka kwa vilabu na sehemu za burudani zilizo karibu na makazi ya watu.

Kupitia kwa Muungano wa Wakazi wa Pwani ya Kusini (SCRA), walisema wanashuku biashara hizo hazina leseni.

Mwenyekiti wa SCRA, Dkt Stan Kinsch, aliitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA), kuongeza wafanyakazi Kwale ili kukabiliana na hali hiyo.

Afisa mkuu wa NEMA, Kaunti ya Kwale, Bw Godfrey Wafula, alithibitisha walipokea malalamishi na wenye biashara hizo tayari wameonywa.

“Ingawa ni serikali ya kaunti ambayo inafaa kushughulikia hilo, tunashirikiana nao ili kuhakikisha kuwa tatizo hili linatatuliwa,” Bw Wafula aliambia Taifa Leo.

Pia alisema wameanza kuwakamata baadhi ya wahusika wa biashara hizo na kuna kesi zinaendelea mahakamani.

Bw Wafula alilaumu hali hiyo kutokana na upangaji mbaya wa ujenzi katika mji wa Diani.

Aidha alisema hivi karibuni wanaandaa mkutano kati ya maafisa wa NEMA, Maafisa wa Serikali ya Kaunti, polisi, chama cha wakazi, viongozi wa kidini na waendeshaji biashara ili kuwe na mashauriano.

“Hatuwezi kuendelea kwenda mahakamani, njia nzuri itakuwa ni kuwa na mkutano wa pamoja ili tuweze kushughulikia suala hilo kwa pamoja,” Bw Wafula alisema.

  • Tags

You can share this post!

Patrick Jungle na Anne Nyokabi waahidi kuwaletea wakazi wa...

Wagonjwa wa figo waomba Kaunti iwasaidie

T L