• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
Patrick Jungle na Anne Nyokabi waahidi kuwaletea wakazi wa Kiambu maendeleo ya kweli

Patrick Jungle na Anne Nyokabi waahidi kuwaletea wakazi wa Kiambu maendeleo ya kweli

NA LAWRENCE ONGARO

MBUNGE wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amemteua Bi Anne Nyokabi Gatheca awe mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro kikali cha kusaka kiti cha ugavana.

Bi Nyokabi aliwahi kuwa Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kiambu kati ya mwaka wa 2013-2017.

Wawili hao watawania kiti hicho wakitumia tiketi ya kujitegemea.

Wengine wanaotamani kiti hicho ni gavana wa Kiambu, Dkt James Nyoro (Jubilee), William Kabogo (Tujibebe Wakenya), Seneta Kimani Wamatangi (UDA), Moses Kuria (Chama cha Kazi), Juliet Kimemia (KANU), na Mwende Gatabaki (Safina).

Bi Nyokabi ni msomi anayeendeleza masomo ya usimamizi wa maswala ya umma katika Chuo Kikuu cha Strathmore jijini Nairobi.

Bw Wainaina alisema alimteua kwa sababu ni kiongozi aliyewahi kujaribiwa na ana ujuzi mwingi wa kuchangia.

“Nilikubali kumteua kwa sababu mawazo yetu yanaambatana pamoja na kwa hivyo tutaweza kufanya kazi ya kuridhisha tukishikana,” alisema Bw Wainaina.

Alieleza kuwa wanalenga kuwaleta watu pamoja ili kufanya biashara zao.

Aliongeza kuwa tayari kiongozi huyo Bi Nyokabi, amevutia vikundi zaidi ya 5,000 vya vijana na wanawake ambapo wataweza kuhamasishwa kwa mafunzo ya biashara kwa kupokea mikopo.

“Mpango huo nimeuendesha kwa zaidi ya miaka 10 na kwa hivyo utawezekana. Ushirikiano wetu utaleta mvuto wa kipekee,” alifafanua Bw Wainaina.

Mbunge huyo alisema maswala muhimu atakayozingatia sana ni afya, kilimo, maji, barabara, na kazi.

Alisema wakazi watahimizwa kuingilia kilimo huku wakitafutiwa masoko ya kupeleka mazao yao.

Bi Nyokabi alisema muungano wake na Bw Wainaina unatokana na rekodi yake safi ambayo ameonyesha zaidi ya miaka kumi akiwa uongozini.

“Nina imani kuwa tutafanya kazi ya kuridhisha wakazi wa Kiambu. Kwa hivyo tunachohitaji ni ushirikiano wa kila mmoja,” alifafanua Bi Nyokabi.

Anasema mbunge huyo ameonyesha mazuri na Sh100 milioni alizopokea kwa matumizi ya maendeleo katika eneobunge na kwa hivyo akipokea mabilioni akiwa gavana atafanya mengi ya kuwaridhisha wakazi.

Naye gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, amemteua Bi June Njambi ambaye ni mtaalam wa maswala ya matibabu.

Alisema kutokana na ujuzi huo wake wataweza kuinua maswala ya kiafya kaunti ya Kiambu.

Dkt Nyoro alijitetea kwa kusema kwamba kwa miaka miwili aliyokuwa uongozini amefanya maendeleo mengi.

Alitaja afya, kilimo, miundomsingi na umeme kama baadhi ya mambo ambayo amelainishia wakazi wa Kiambu.

Bw William Kabogo naye alimteua Bi Esther Ndirangu, kama naibu wake katika kuwinda kiti cha ugavana.

Alimtaja kama msomi aliyefuzu kwa uzamifu katika elimu.

Alisema ujuzi huo utakuwa muhimu wakiungana pamoja kuinua maendeleo Kiambu.

Mbunge wa Gatundu Bw Moses Kuria naye alimteua Bi Faith Mwaura ambaye ni mfanyabiashara wa maswala ya ujenzi wa majumba makubwa.

Alisema tayari wamejipanga vilivyo kuzindua kampeni yao ili kuzunguka kaunti yote ya Kiambu wakitafuta kura.

  • Tags

You can share this post!

Thika Queens bado yalenga kukamilisha kampeni miongoni mwa...

Walalamikia kelele za maeneo ya burudani katika mitaa ya...

T L