• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 12:41 PM
Walimu wa shule za msingi wafungiwa nje kusimamia KCSE

Walimu wa shule za msingi wafungiwa nje kusimamia KCSE

Na WAANDISHI WETU

WALIMU wa shule za upili pekee ndio wataruhusiwa kusimamia mitihani ya kitaifa ya sekondari (KCSE), amesema mkurugenzi mkuu wa Tume ya Huduma kwa Walimu nchini (TSC) Bi Nancy Macharia.

Bi Macharia alisema kanuni za mtihani wa kitaifa haziruhusu walimu wa shule za msingi kusimamia mtihani huo.

Bi Macharia aliyesimamia kufunguliwa kwa kontena ya mitihani mjini Mombasa aliwahimiza walimu kusimamia mitihani kwa njia ya uaminifu.

“Walimu wa shule za msingi hawawezi kusimamia mitihani ya KCSE. Wanakubaliwa tu kusimamia mitihani ya kitaifa ya shule za msingi pekee,” alisema Bi Macharia.

Watahiniwa 52, 958 wa mtihani wa Cheti cha Elimu ya Sekondari (KCSE) Pwani walianza mtihani wao hapo jana huku mvua ikiendelea kunyesha katika maeneo tofauti Pwani.

Mitihani mikuu ya KCSE ilianza Novemba 6, 2023 asubuhi kwa karatasi ya mtihani wa Kemia.

Mkurugenzi wa Elimu eneo la Pwani, Lucas Kangongo alisema kuwa licha ya mvua kubwa iliyonyesha tangu Ijumaa, Wizara ya Elimu imehakikisha kwamba mitihani imefika katika kila kituo.

“Tulichukua hatua ya haraka kabla ya hali kuwa ngumu zaidi. Huko Tana River, kulikuwa na mvua nyingi na baadhi ya vituo vya mitihani havikuweza kufikiwa kwa hivyo ilitubidi kutafuta usaidizi kutoka kwa Baraza la Mitihani nchini (KNEC) ambalo lilitoa ndege kutumika Tana River,” alisema mkuu huyo wa elimu.

Bw Kangongo alisema Tana Delta pia iliathiriwa na kulazimisha Wizara ya Elimu kuhamisha vituo viwili vya mitihani hadi eneo jingine salama.

Huko Taita Taveta, Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Bw Khalif Hirey, alisema kuna usalama wa kutosha na vifaa ili kuhakikisha mchakato wa mitihani unafanyika vizuri.

Mkurugenzi wa Elimu Kaunti ya Lamu, Zachary Mutuiri aliambia Taifa Leo kwamba mitihani ilianza vizuri sana bila kisa cha utoro miongoni mwa watahiniwa walioripoti kote katika kaunti hiyo.

Akifungua kontena ya mitihani hiyo huko Matuga, Kamishna wa Kaunti ya Kwale Michael Meru alisema visa vyovyote vya udanganyifu vitakavyoripotiwa vitachunguzwa kikamilifu na hatua faafu kuchukuliwa.

Katibu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Hassan Abubakar mnamo Jumatatu aliongoza ufunguzi wa kontena ya mitihani katika mji wa Kale wa Lamu, aliwasihi watahiniwa kutia bidii ili wapate matokeo bora mwaka huu. Kaunti ya Lamu ina jumla ya watahiniwa 2,309 wa KCSE ambao wote jana walianza mtihani wao vyema.

Kwa mujibu wa ofisi ya Elimu, Lamu, eneo hilo lina jumla ya vituo 34 vya KCSE ambapo wanafunzi wanafanyia mtihani huo mwaka huu.

Mkurugenzi wa Elimu, kaunti ya Lamu, Zachary Mutuiri aliambia Taifa Leo kwamba kinyume na miaka iliyopita ambapo Lamu ilishuhudia vimbwanga, ikiwemo baadhi ya watahiniwa kujifungua ilhali wengine wakiufanyia mtihani huo hospitalini, mwaka huu hali ni shwari kwani wanafunzi walianza mitihani yao ilivyotarajiwa bila kisa chochote kushuhudiwa.

Bw Mutuiri aliishukuru serikali kuu kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani kwa kuhakikisha usalama dhabiti kila mahali wakati KCSE ikiendelea.

Afisa huyo aliwaonya wazazi, wanafunzi, walimu na hata maafisa wa usalama dhidi ya kujihusisha na visa vyovyote vya udanganyifu.

Ripoti za Cece Siago, Lucy Mkanyika, Stephen Oduor, Kalume Kazungu na Winnie Atieno

  • Tags

You can share this post!

Ole wako wewe mwenye kutumia simu msalani!

Nashindwa kumsaidia mwanamume mpenzi wangu kifedha kwa...

T L