• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Walimu wataka Kilifi iorodheshwe kuwa mazingira magumu ya kufanyia kazi wapokee marupurupu ya maana

Walimu wataka Kilifi iorodheshwe kuwa mazingira magumu ya kufanyia kazi wapokee marupurupu ya maana

NA MARY WANGARI

WALIMU zaidi ya 2,000 wamewasilisha malalamishi kwa Seneti wakitaka Kaunti ya Kilifi kuorodheshwa kama eneo kame na mazingira magumu ya kufanyia kazi.

Wanataka walimu katika eneo hilo kulipwa marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira magumu yakiwemo marupurupu ya nyumba kwa baadhi ya walimu walioajiriwa na Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) katika kaunti hiyo.

Wamesema kuwa licha ya kaunti yote ya Kilifi kuwa eneo kame, TSC imekuwa ikizingatia tu maeneo ya Magarini na Ganze.

Kupitia Muungano wao wa Walimu wa Shule za Sekondari Nchini (Kuppet), walimu hao wameishutumu TSC kwa kuzingatia walimu katika maeneo mawili pekee huku ikiwapuuza wale wengine.

“Kaunti yote ya Kilifi ni eneo kame lakini inasikitisha kuwa TSC ilizingatia tu maeneo ya Magarini na Ganze huku maeneo mengine yakitengwa,” akasema Katibu Mkuu wa Kuppet, tawi la Kilifi Bw Caleb Mogere.

Akaongeza: “Idadi kubwa ya wasimamizi wa shule katika Kaunti ya Kilifi wanashikilia nyadhifa za ukaimu hivyo kushusha motisha wa walimu hawa wanaopaswa kunufaika kutokana na mpango wa usawazishaji.”

Walilalamika kuwa walimu katika maeneo kama vile Kaloleni, Chonyi, Rabai, Shule za Msingi na Sekondari za Marafiki na Shule ya Sekondari ya Uyombo Girls hawapokei marupurupu, licha ya maeneo hayo kuorodheshwa kama mazingira magumu kikazi kutokana na ukosefu wa huduma na vituo vya kijamii.

Isitoshe, wanaitaka TSC kuwapa walimu marupurupu ya makazi kila mwezi wakisema kuwa “marupurupu haya hupatiwa walimu wa kudumu hata ingawa huwa hawapati kiasi sawa. Malipo hayo yanajikita kwenye vigezo viwili: daraja la mwalimu kikazi na kituo cha kazi.”

Nao walimu wa chekechea (P1 Level A) wameitaka Seneti kuingilia kati ili kuwawezesha kulipwa malimbikizo ya mishahara yao ya miaka 27 iliyopita (kati ya 1996 na 2010).

Walihoji kuwa mnamo Mei 1996, Wizara ya Elimu, ilipandisha daraja la walimu wa Kiwango cha UTS A kuwa SI baada ya kuhudhuria kozi ya wiki mbili katika Vyuo vya Mafunzo ya Walimu Kagumo na Bondo huku ikiwatenga walimu waliopokea mafunzo ya Kiwango cha A P1.

Ikijitetea hata hivyo, TSC imesema uorodheshaji wa maeneo kame ni jukumu la Wizara ya Huduma ya Umma, huku Tume ya Kutathmini Mishahara na Marupurupu (SRC) ikiwa na wajibu wa kutoa ushauri kuhusu malipo na marupurupu ya watumishi wa umma, wakiwemo walimu.

  • Tags

You can share this post!

Raia wa Rwanda na Mkenya wafika kortini...

Madereva wa masafa marefu wahamasishana, waombea nafsi za...

T L