• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Walioingiza raia wa Ethiopia watozwa faini ya Sh60 milioni

Walioingiza raia wa Ethiopia watozwa faini ya Sh60 milioni

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA na dereva wake wametozwa faini ya Sh60 milioni ama watumikie kifungo cha miaka 10 gerezani kwa ulanguzi wa binadamu.

Ali Mitano na Abdinasir Walde walisukumiwa hukumu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuwaingiza nchini raia 11 wa Ethiopia waliokuwa wanaelekea Afrika Kusini.

Hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi aliwatapa na hatia Mitano na Walde kisha akamwachilia huru Mohamed Makura Walde, nduguye Abdnasir.

“Hii mahakama imewapata na hatia ya kuwaingiza nchini raia 11 wa Ethiopia kutoka Mandera mkijua walikuwa wanaenda kunyanyaswa, ”alisema Bw Ochoi.

Mahakama ilisema Mitano, Abdinasir na Makura hufanya kazi ya kusafirisha maziwa kutoka Nairobi hadi Moyale, mji ulio kwenye mpaka wa Kenya na Ethiopia.

Walishtakiwa kwamba mnamo Julai 9, 2019 katika eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a, waliwalangua raia 11 wa Ethiopia, waliowasafirisha ndani ya lori nambari KBZ 577E kwa nia ya kuwanyanyasa.

Mahakama iliambiwa kwamba raia hao walikuwa wamefungiwa ndani ya kontena maalum.

Kontena hiyo maalum ilikuwa imewekwa mahala pa kuingizia hewa.

Raia hao walikuwa wamefungiwa mle ndani.

“Polisi walisimamisha lori hili na baada ya kulikagua wakawapata raia hao wa Ethiopia,” alisema Bw Ochoi.

Ushahidi uliotolewa mahakamani ni kuwa raia hao wa Ethiopia walipigiwa simu watembee kwa miguu hadi Moyale ambapo waliabiri lori hilo.

Walalamishi hao walisema ajenti ambaye angaliwasafirisha hadi Afrika Kusini alichukua pasipoti zao na pesa kisha wakazuiliwa ndani ya chumba.

Mmoja wa raia hao, Wondimu Worko, alisema mnamo Juni 2018 alipokea simu kutoka Afrika Kusini ambapo aliahidiwa kazi.

Worko aliagizwa asafiri hadi Moyale ambapo alichukuliwa kwa lori na kukamatwa Makuyu wakielekea Nairobi.

Ijapokuwa Mitano na Walde walisema walikuwa wamewasaidia raia hao wa Ethiopia kufika Nairobi, Bw Ochoi alisema wawili hao walikuwa wakifanya biashara hiyo ya kuwasafirisha raia hao katika kontena maalum.

“Hii mahakama imewapata na hatia ya kuwalangua raia wa kigeni. Kila mmoja atalipa faini ya Sh30 milioni ama kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani,” alisema Bw Ochoi akiwahukumu.

You can share this post!

Kinara wa UoN kusomewa hukumu Januari 22 kwa kuidharau...

Kidero, Orengo wahudhuria Azimio La Umoja badala ya korti

T L