• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Walioteleza KCPE wawika katika KCSE

Walioteleza KCPE wawika katika KCSE

Na CECIL ODONGO

BAADHI ya wanafunzi ambao walipata alama za chini katika mtihani wa KCPE mnamo 2016 ni kati ya wale waliong’aa kwenye mtihani wa KCSE uliotolewa jana na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha.

Wanafunzi hao ambao pia walijiunga na shule za kaunti ambazo si za hadhi ya juu, sasa watajiunga na vyuo vikuu baada ya kupata alama ya C+. Isitoshe baadhi ya wanafunzi hao walipata chini ya alama 200 lakini wakajikaza masomoni na kuibuka kidedea.

Abdullahi Daud Maalim aliyepata alama 136 pekee katika mtihani wa KCPE 2016, alishangaza baada ya kupata alama ya C+.

Maalim alikuwa akisomea shule ya upili ya Ademasajida katika Kaunti ya Wajir. Musharaf Kerow Adan kutoka Shule ya sekondari ya Mandera pia alipata alama ya C+ japo katika mtihani wa KCPE alipata alama 140 pekee.

Wengine waliopata alama za chini KCPE na kuhitimu kujiunga na vyuo vikuu ni Hassan Abdullahi Osman aliyepata B- (168), Cheruyot Bett B- (190), Maluti Tom B- (199), Kipees Charity C+ (151) na Shadera Salvin (168) B- kutoka shule za Wayam Seco, Kimargis, St Teresa Bikeke na Olderkesi mtawalia.

Wanafunzi wengine ni Kamar Jimale B-(163), Ruweitha Hassan B- (193) na Siololo Joseph B-(186) kutoka shule za Habaswein, Hon Khalifa Girls na Olderkesi mtawalia.

“Matokeo haya ya wanafunzi waliofanya vibaya KCPE na wakafuzu kujiunga na vyuo vikuu ni ishara kwamba mpango wa serikali wa wanafunzi wote kujiunga na shule za upili umefanikiwa. Tukiendelea na mpango huu tutawanusuru wanafunzi wengi waliodhaniwa hawatapata matokeo mema kwa kufeli KCPE,” akasema Prof George Magoha akitangaza matokeo hayo.

Aidha baadhi ya shule zilizowasajili wanafunzi wenye alama za chini na kung’aa kwa KCSE ni Kaaga Girls ambayo ilikuwa na alama ya 73.98 kutoka 22.38, St Joseph Kitale 71.57 kutoka 21.22, Kisasi 68.25 kutoka 20.43, Oriwo ilipata alama 78.72 kutoka 31.07 na Riokindo 65.23 kutoka 18.13.Shule nyingine ni St Joseph Rapogi (77.78), Light Academy (76.74), Moi Gesusu (70.89), Saye (70.09), Wiobiero (70.04)), Chuka (69.24), Strathmore (69.57) Bushra (63.51) na Mahiga Girls (63.95)

You can share this post!

Shule za Pwani zakosa kung’aa KCSE

Viongozi Pwani watafutia Ruto mgombea mwenza