• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Wanafunzi wa chuo cha ufundi Thika kuhusika moja kwa moja katika utengenezaji magari

Wanafunzi wa chuo cha ufundi Thika kuhusika moja kwa moja katika utengenezaji magari

NA LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI katika chuo cha Thika Technical Vocational Training Centre watapata nafasi ya kuunda sehemu za magari katika chuo hicho.

Mipango hiyo ni kutokana na ushirikiano wa Kenya na Ujerumani ili wanafunzi wawe na ufahamu na ujuzi wa kazi za mikono.

Baadhi ya kozi zitakazoendeshwa katika chuo hicho ni ya Mechatronic, Automation Mechatronics, huku pia wakichomelea vyuma na kurekebisha injini za magari.

Kulingana na naibu mkurugenzi wa kitengo cha masuala ya ufundi na teknolojia John Tuwei, ni kwamba baada ya wanafunzi hao kupata mafunzo ya ufundi watakabidhiwa cheti maalum cha hapa nchini na cha Ujerumani.

“Hiyo ni njia moja ya kuwaweka katika hadhi ya juu na pia itakuwa inawapa nafasi nzuri ya kupata kazi,” alisema Bw Tuwei.

Alieleza pia kuwa wanafunzi hao watapata nafasi ya kuendesha ujuzi wao katika viwanda tofauti ili wapate ujuzi zaidi wa kazi.

Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa sababu watatambulika kwa haraka wanapojiwasilisha popote kutafuta kazi.

Wanafunzi wa chuo cha ufundi Thika kuhusika moja kwa moja katika utengenezaji magari. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Aliyasema hayo mnamo Jumanne katika chuo hicho walipozindua ujenzi wa madarasa yatakayotumika katika uundaji wa sehemu za gari.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a aliridhika na mpango huo akisema vijana wengi kutoka eneo lake watapata ujuzi na pia nafasi za kazi wakikamilisha kozi hiyo ya ufundi.

“Ni jambo la kufurahisha kupata ya kwamba mji wa Thika utarejelea sifa zake za hapo awali kama mji wenye viwanda vingi nchini,” alisema mbunge huyo.

Alisema vijana wengi waliokamilisha kozi zao watakuwa na nafasi njema ya kupata ajira kwa sababu wengi wao watakuwa na ujuzi kwenye viwanda kadha vya hapo Thika.

“Mimi kama mbunge wa Thika ninawahimiza wazazi kuwarai vijana wao wazingatie kozi za ufundi ili baada ya kukamilisha waweze kupata nafasi za ajira,” alifafanua Bi Ng’ang’a.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wakuu katika serikali wakiongozwa na naibu kamishna Bw Mbogo Mathioya, na walimu wanaosimamia kitengo cha ufundi katika chuo hicho.

  • Tags

You can share this post!

Raila hatarini kusalia pweke katika upinzani

Arsenal wakomoa Wolves ugenini na kufungua mwanya wa alama...

T L