• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Wanaharakati walaani hatua ya wanawake Lamu kufungiwa milango jeshini

Wanaharakati walaani hatua ya wanawake Lamu kufungiwa milango jeshini

NA KALUME KAZUNGU

WANAHARAKATI wa kijamii na miungano ya akina mama kaunti ya Lamu imelaani vikali kuzuiliwa kwa wanawake wa tarafa za Hindi na Amu dhidi ya kushiriki zoezi la kusajili makurutu kuingia Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

Shughuli hiyo iling’oa nanga mapema Jumatatu kwenye uwanja wa Kibaki Grounds kisiwanmi Lamu.

Aidha, mamia ya wanawake waliojitokeza kutafuta nafasi hizo adimu jeshini walivunjika moyo baada ya Afisa Mkuu Msimamizi wa Usajili wa Makurutu stesheni ya Amu, Luteni Kanali Hamisi Msagha kuwaomba radhi ya mapema wanawake hao kwani hawatachukuliwa kwenye awamu ya usajili ya mwaka huu ya Lamu.

Katika mahojiano na Taifa Dijitali, Bw Msagha alieleza wazi sababu zilizopelekea wanawake wa Lamu kunyimwa fursa ya kushiriki zoezi la kusajiliwa kwa makurutu kuingia jeshini, akitaja kuwa kulingana na takwimu za kitaifa, Lamu iko na uwakilishi wa kutosha wa wafanyakazi wa kike jeshini.

“Kwa leo wanawake wa Amu na Hindi watatuwia radhi kwani hawatazingatiwa kamwe katika usajili wa makurutu kuingia jeshini mwaka huu. Huwa tunazingatia kiwango au idadi tuliyopewa katika kila eneo. Tukitazama tunaona takwimu za Lamu zikiashiria kuwa kuna uwakilishi wa kutosha wa watendakazi wa jinsia ya kike jeshini. Hii ndiyo sababu leo tunachagua na kusajili wanaume pekee,” akasema Bw Msagha.

Hatua hiyo hata hivyo haijawafurahisha wengi, hasa wanaharakati wa kijamii wanaoshikilia kuwa ni makosa kikatiba kuinyima jinsia moja usajili katika kazi, hasa serikalini.

Msemaji wa Muungano wa Maendeleo ya Wanawake, Kaunti ya Lamu, Hindu Salim, alihoji kuwa Rais William Ruto kila wakati amekuwa akisisitiza kwamba lazima wanawake wapewe kipaumbele, hasa katika kazi nchini.

Bi Salim alieleza kushangazwa kwake na wanawake wa kisiwa cha Lamu na Hindi kunyimwa fursa ya kusajiliwa jeshini, akiitaja kauli ya Afisa Mkuu wa Usajili kwamba Lamu ina wanawake wa kutosha jeshini kuwa kinaya.

“Kamwe sijaridhishwa na kuzuiwa kwa wanawake kushiriki shughuli ya kusajiliwa jeshini hapa kisiwani Lamu leo. Kwa nini kauli ya Rais Ruto kwamba angezingatia sana jinsia ya kike katika uajiri wa kazi nchini unakiukwa? Ni takwimu gani hizo zinazodai eti Lamu kuna uwakilishi wa kutosha wa jinsia ya kike jeshini? Hicho ni kinaya. Ningeomba serikali itupe kipaumbele sisi wanawake, hasa hapa Lamu katika kazi za serikali kwani bado tuko nyuma,” akasema Bi Salim.

Naye Bi Fatma Omar, ambaye ni mwanachama wa Sauti ya Wanawake wa Lamu, aliisihi serikali miaka ijayo pia kuwanyima wanaume nafasi ya kushiriki usajili eneo hilo ili fursa hiyo iendee wanawake pekee.

Bi Omar alihoji kwa nini wanawake wa Lamu kila mara wanazuiliwa katika kusajiliwa kuingia jeshini.

Mnamo Novemba, 2018, wanawake wa Lamu waliokuwa wamejitokeza kujitafutia nafasi za kusajiliwa jeshini walirudi nyumbani wakiwa wamevunjika mioyo baada ya kuarifiwa kwamba usajili huo haukuwazingatia.

“Sasa imekuwa mtindo kila mara kwamba wanawake hawahitajiki jeshini. Si mara ya kwanza wanawake kufanywa hivi hapa Lamu. Ni matumaini yangu kwamba miaka ijayo pia jinsia ya kiume itafungiwa nje ili wanawake nao washiriki usajili wa kuingia jeshini peke yao,” akasema Bi Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Lamu Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau aliitaka serikali kuziweka wazi takwimu zinazodai kwamba Lamu ina uwakilishi wa kutosha wa wanawake wanaohudumia jeshi la Kenya.

“Tumechoka na huo ubaguzi wa kila siku. Inahuzunisha kuona wanawake wetu wameamka alfajiri, kuvunja itikadi za dini na zile za kijamii na kufika uwanjani ili wasajiliwe na kisha wanazuiwa. Tunataka hizo takwimu zinazosemekana kwamba Lamu ina wanawake wa kutosha jeshini ziwekwe wazi-paruwanja. Hatufurahii haya yanayoendelea. Si haki kamwe,” akasema Bi Famau.

Mmoja wa makurutu wa kike waliojitokeza na kisha kukatazwa kushiriki zoezi hilo la usajili, Bi Rose Mukami alieleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo.

Bi Mukami ambaye ni mkazi wa Hindi, karibu kilomita 60 kutoka kisiwa cha Lamu, alirauka na kufika kisiwani Lamu kwa wakati, akiwa mwingi wa matumaini kwamba angeweza kufaulu kuingia jeshini leo.

Bi Mukami ana umri wa miaka 26, hivyo mwaka ujao hataweza kushiriki shughuli ya usajili wa makurutu kwani atakuwa amepitisha umri.

“Nimefuzu mafunzo ya vijana kwa taifa (NYS). Niko na miaka 26 na huu ulikuwa ndio mwaka wangu wa mwisho kwamba niweze kusajiliwa jeshini. Wanawake tumenyimwa fursa kushiriki. Hii inamaanisha umri wangu utakuwa umesonga kufikia mwaka ujao. Nasikitika kwamba ndoto yangu ya kuingia jeshini inazidi kukandamizwa,” akasema Bi Mukami.

  • Tags

You can share this post!

Mhadhiri atiliwa ‘mchele’, agundua kilabuni kuna walimu...

Vijana wa Eldoret walioahidiwa kazi nchini Qatar wataka...

T L