• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Washukiwa 12 wa genge la Wakali Kwanza wajisalimisha

Washukiwa 12 wa genge la Wakali Kwanza wajisalimisha

Na FARHIYA HUSSEIN

VIJANA 12 wanaoshukiwa kuwa wa genge la ‘Wakali Kwanza’ wamejisalimisha kwa maafisa wa polisi Kaunti ya Mombasa.

Vijana hao ambao wengi wao wako chini ya umri wa miaka 18 na wengine katika umri wa miaka ya 20 walijisalimisha katika kituo cha polisi cha Nyali wakiwa pamoja na Mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Nyali Daniel Mumasaba alisema uchunguzi wa ndani utaanzishwa kwa waliojisalimisha.

“Tulishirikiana na wazee wa mtaa pamoja na wakazi tukaanzisha msako ndiposa vijana hawa wameamua kujisalimisha na kuachana na maisha ya uhalifu,” akasema Bw Mumasaba.

Genge la ‘Wakali Kwanza’ linaogofya sana katika maeneo ya Nyali, Kisauni, Likoni, Mvita na Bamburi ambapo wahalifu hao wanajulikana kwa kutisha wakazi.

Wanajulikana zaidi kwa kuwapiga risasi na kuwadunga visu waathiriwa wakati wa ujambazi.

“Nimeamua kujitokeza leo kwa kuwa tumehakikishiwa usalama wetu. Uhalifu umekuwa maisha yangu kwa zaidi ya miaka sita,” alisema Hamisi Mwalimu, mmoja wa waliojisalimisha.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 27, analaumu maisha yake ya uhalifu akisema kisababishi kikuu ni kutengana kwa familia yake akisema amewahi kukamatwa mara moja na kufungwa katika Gereza la Shimo la Tewa, lakini baadaye akaachiliwa kwa dhamana ya pesa.

“Nina mke na watoto wanne na ndiyo sababu kuu nimeamua kujisalimisha. Marafiki zangu wengi wameuawa wakati wengine bado wako kwenye maisha ya uhalifu. Natumai watapata njia ya kutoka kabla hawajachelewa,” alisema.

Mwenzake Rajab Rama Konde ambaye anajulikana zaidi kama ‘One Man Army’ anasimulia jinsi alivyoachiliwa hivi karibuni kutoka jela.

Amelaumu maisha yake ya uhalifu kwa uraibu wa dawa za kulevya.

“Ninapoiba au kumuibia mtu ninachofanya na pesa hizo ni kununua dawa za kulevya,” alikiri.

Rama anasema alianza kujihusisha na uhalifu wakati alikuwa na umri wa miaka 17.

“Nimekamatwa mara mbili. Mara ya kwanza nilizuiliwa kwa miezi tisa katika Gereza la Shimo la Tewa na mara ya pili nilikuwa nikitumikia kifungo cha mwaka mmoja,” akasema.

Kulingana na mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu mjini Mombasa, Mahmoud Noor, vijana zaidi ya 250 wamejisalimisha kufikia sasa na kusaidiwa kuanzisha miradi tofauti tofauti.

“Tayari tumesaidia zaidi ya vikundi 11 ambapo wengine wamepokea pikipiki, vifaa vya uvuvi na wengine wamejitoza katika ufugaji wa kuku,” alisema.

Bw Mumasaba alilaumu wazazi kwa kupuuza watoto wao na kuwaruhusu kujihusisha na maisha ya uhalifu.

You can share this post!

Bunge la Vihiga kujadili iwapo mawaziri wanne watimuliwe au...

Uhuru atikisa demokrasia