• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Watetea kauli ya Raila kutoteua mwaniaji urais

Watetea kauli ya Raila kutoteua mwaniaji urais

Na JUSTUS OCHIENG’

MATAMSHI ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa hatawaunga mkono vinara wenzake katika Muungano wa Nasa, umetikisa anga za siasa nchini na kuvutia mseto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga aliweka mambo wazi mnamo Jumamosi katika hafla ya mazishi eneobunge la Ndhiwa, Kaunti ya Homa Bay, akisema vinara wenzake walimsaliti baada ya kuingia mitini wakati wa kuapishwa kwake kama Rais wa wananchi mnamo Januari 30, 2018.

Kauli ya Bw Odinga iliwachemsha Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) ambao wamekuwa wakitoa wito kwamba asitishe azma yake ya urais 2022 kisha amuunge mkono mmoja wao.

Hapo jana, wandani wa Bw Odinga katika chama cha ODM walijitokeza na kumtetea kinara wao, wakisema hana nafasi ya kuwavumilia au kujihusisha na viongozi waoga ambao walimsaliti wakati ambapo aliwahitaji mno.

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi na mwekahazina wa chama hicho Timothy Bosire, Jumatatu walisema kuwa Bw Odinga atawania Urais mnamo 2022 wala hatawaunga mkono vinara wenzake wasaliti.

Ingawa Bw Odinga mwenyewe bado hajasema wazi kuwa atakuwa debeni, kauli ya wandani wake inaashiria kuwa kigogo huyo wa siasa za upinzani nchini atakuwa akijaribu bahati yake kwa mara ya tano debeni.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa nao wamekuwa wakisema waziri huyo mkuu wa zamani yupo pazuri kuingia ikulu kutokana na ukuruba wa kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta maarufu kama ‘handisheki’.

“Ndiyo watu wanachukia Raila lakini mtu asikudanganye kuwa hahitaji uungwaji mkono wake. Bw Odinga amevumilia mawimbi makali ya kisiasa na amedumisha wafuasi wake kutokana na mtindo wa kipekee wa siasa zake,” akasema Bw Mbadi.

Bw Bosire naye alisema kuwa Bw Odinga ndiye mwanasiasa mwenye hadhi zaidi nchini baada ya Rais Kenyatta na ndiye bora zaidi kutwaa uongozi wa nchi mnamo 2022.

“Ndiye mwanasiasa ambaye anaweza kuendesha kampeni zake kivyake. Amekuwa akishinda chaguzi za nyuma na hata kuonekana kama Rais na wafuasi wake bila kuzingatia utawala uliopo mamlakani,” akasema Bw Bosire.

Mwanasiasa huyo pia alimsifia Bw Odinga kutokana na kuboresha miundomsingi alipokuwa waziri wa barabara katika utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki na kama Waziri Mkuu ndani ya serikali ya muungano.

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa Mark Bichache na Donald Mokua, Bw Odinga ameweza kujidumisha katika siasa za taifa na hata akihiari kutowania Urais bado atakuwa na usemi mkubwa kuhusu anayefaa kumrithi Rais Kenyatta.

“Hakuna mwaniaji yeyote ambaye anaweza kupata kura ambazo Bw Odinga atapigiwa bila kuingia kwenye muungano na wagombeaji wengine. Japo alikuwa akikashifiwa kwa msingi wa umri, hilo sasa halina mashiko tena kwa sababu hata Rais wa Marekani Joe Biden ni mzee,” akasema Bw Bichache.

“Akipata tu kura chache katika eneo la Kati ataingia ikulu na hilo linawezekana kutokana na ushirikiano kati yake na Rais Kenyatta,” akaongeza.

Bw Mokua naye alisema nafuu kwa Bw Odinga ni umaarufu anaojivunia nyanjani na katika miji mikubwa nchini, ambao wawaniaji wengine hawana.

You can share this post!

Kidero akemea wanaovuruga mikutano

BI TAIFA FEBRUARI 23, 2021