• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 12:05 PM
Watu 18,000 waokolewa kwa meno ya Taliban

Watu 18,000 waokolewa kwa meno ya Taliban

NA AFP

IDADI ya watu walioondolewa nchini Afghanistan imefikia 18,000 huku hofu ikizidi kuongezeka baada ya wanamgambo wa Taliban kuanzisha operesheni ya nyumba kwa nyumba kusaka wanaoshirikiana na ‘maadui’ wao.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) inaonyesha kuwa wanamgambo wa Taliban wanalenga raia wa Waafghanistan walioshirikiana na wanajeshi wa Amerika na majeshi ya muungano wa Amerika na Ulaya (NATO).

“Taliban pia wanalenga familia za watu wanaosakwa; wakikwepa mtego wao wanaenda kuhangaisha familia zao,” ikasema ripoti ya UN.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Amerika inaonyesha kuwa tangu Agosti 14, wanamgambo wa Taliban walipopindua serikali ya Afghanistan, wanajeshi wa Amerika wamewaokoa watu 9,000.Wanajeshi wa NATO walisema nchi mbalimbali zimefanikiwa kuokoa jumla ya watu 18,000 na misongamano ya watu inaendelea kushuhudiwa katika uwanja wa ndege wa Kabul.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Wakimbizi (UNHCR) jana liliyataka mataifa jirani na Afghanistan kufungua mipaka ili kuwezesha watu wanaotoroka Taliban kuingia.Msemaji wa UNHCR, Shabia Mantoo, alisema kuwa idadi kubwa ya Waafghanistan hawana uwezo wa kutoroka nchi hiyo kwa kutumia ndege.

“Tunasihi nchi jirani kufungua mipaka kuwezesha watu kuingia na kutafuta hifadhi,” akasema Mantoo. Kundi la Taliban lenye msimamo mkali wa Kiislamu limejaribu kuwahakikishia Waafghan tangu kutwaa madaraka, kuwa hakutakuwa na ‘kisasi’.

Taliban waliudhibiti mji wa Kabul Jumapili, baada ya kupindua serikali ya nchini hiyo. Ushindi wao unarudisha kundi hilo madarakani baada ya miaka 20 tangu wang’olewe katika operesheni iliyoongozwa na Amerika.

Wakati wa utawala wa Taliban miaka 20 iliyopita, visa tele vya dhuluma na mauaji vilishuhudiwa huku wanawake wakibaguliwa.Lakini katika mkutano wao wa kwanza wa waandishi wa habari tangu kuchukua tena udhibiti wa Afghanistan, kundi hilo liliahidi haki za wanawake zitaheshimiwa ‘kwa kuzingatia sheria ya Kiislamu’.

Taliban wameripotiwa kuahidi kutowalazimisha wanawake kuvaa burka -vazi linalofunika uso na mwili. Badala yake, hijab – au kitambaa cha kichwa – kitakuwa cha lazima.

Taliban wameruhusu wanaume kuendelea kucheza mchezo wa kriketi lakini hawajatoa tamko lolote kuhusu michezo ya wanawake.

Viongozi wa Taliban jana waliruhusu wanamgambo wake kwenda misikitini kuswali pamoja na raia. Miongoni mwa nchi ambazo zimetuma ndege nchini Afghanistan kuokoa raia ni Indonesia ambayo jana ilisema kuwa imefanikiwa kuondoa watu 26.

You can share this post!

Watanzania wawili kizimbani kwa shtaka la kuiba chupi

Serikali yapewa siku 7 kuzuia mgomo wa wahadhiri