• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Waume walia vijana wa NYS wanawapokonya wake zao kiholela

Waume walia vijana wa NYS wanawapokonya wake zao kiholela

Na STEPHEN ODUOR

WAKAZI wa Kaunti ya Tana River wamewashutumu maafisa wa shirika la Huduma ya Taifa kwa Vijana (NYS) wanaosimamia shughuli ya Kazi Mtaani, wakidai wananyakua wake za watu.

Kulingana na wakazi, vijana hao wa NYS wamekuwa wakiwatongoza wanawake walioolewa, na kusababisha waume kukosewa heshima na mabibi zao.

Wanaume walilalamika kuwa maafisa hao, ambao pia wametwikwa majukumu ya kugawanya kazi, wamekuwa wakichagua maeneo yaliyojitenga kichakani, ambapo hushiriki ngono na wanawake hao.

“Mambo haya yote yalipoanza, mke wangu alikuwa akirudi nyumbani kufikia saa kumi na moja jioni, kisha akaanza mtindo wa kurejea saa moja usiku ambapo niligundua alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msimamizi, ambaye ni mhudumu wa NYS,” alisema Bw Hussein Juma.

Naibu Kamishna wa Kaunti, Geoffrey Mwachofi alieleza kwamba, kumekuwa na minong’ono kimya kimya kuhusu suala hilo, ingawa hakuna mwanamume yeyote aliyewasilisha malalamishi rasmi kwa mamlaka husika.

“Tumekuwa tukisikia malalamishi haya mitaani na huenda kuna mahusiano haramu kama hayo, lakini hawa ni watu wazima. Tulipoajiri, tuliajiri vijana wanaojukumika na wanaoweza kufanya kazi wakiwa na usimamizi mdogo,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kwamba suala hilo litashughulikiwa kwa njia bora iwezekanavyo kuhakikisha hakutakuwa na uhasama baina ya wahudumu hao na wenyeji.

Aidha, aliwahimiza wasimamizi wa NYS kudumisha nidhamu ya hali ya juu na kutekeleza majukumu waliyotengewa kwa ustaarabu.

Isitoshe, wakazi walisema maafisa hao wamekuwa wakiwatumia vibaya wanawake hao, ambao ni nadra kutumia mapato yao nyumbani pindi wanapolipwa.

“Niliamua kufuatilia nambari ya MPesa ambayo mke wangu aliitumia pesa. Niliifuatilia hadi kwa mhudumu wa NYS ambaye nilimkabili karibu tutwangane. Tangu siku hiyo nimempiga marufuku mke wangu kwa kazi hiyo,” alisema Bw Hassan Moroa.

  • Tags

You can share this post!

Ndani miaka 10 kwa kumuumiza mpenziwe

Wakazi wahepa hotuba ya Rais mazishini Gatundu