• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Wazee wampa kijana marufuku ya muda kwa kunywa pombe kabla haijatakaswa

Wazee wampa kijana marufuku ya muda kwa kunywa pombe kabla haijatakaswa

NA SAMMY WAWERU 

KUNDI moja la wazee Nairobi limempa barobaro marufuku ya mwezi mmoja kutokunywa nao pombe, kwa kubugia kileo kabla hakijatakaswa. 

Kwa kawaida, kundi hilo linalojivinjari kwenye mabaa ya mitaa kadha Thika Road, Nairobi hutakasa pombe kabla ya kuinywa.

Wikendi, jamaa huyo aliungana na wazee hao kuondoa mwasho wa koo na alitakiwa kuwafungulia kinywaji.

Kwa pupa, alitia pombe kwenye glasi na kuanza kunywa jambo ambalo lilighadhabisha wazee.

“Wewe sisi tumekula chumvi, na huwa hatufanyi mambo kienyeji. Kabla kileo kuingia mdomoni, lazima kitakaswe,” Mzee Benson Wamalwa aliwakia kijana huyo.

Kulingana na kundi hilo, mvinyo ukishafunguliwa unapaswa kuwekwa kiasi kwenye glasi na kumwagwa huku aliyetwikwa jukumu akikariri maneno ya kuutakasa.

“Hawa vijana wa siku hizi wamevimba kichwa sana…Wazee tunafanya mambo kwa utaratibu, hatutaacha mila, itikadi na desturi zetu za Kiafrika,” Mzee mwingine kwa jina Charles Mwangi alisema.

Sababu hasa za kutakasa pombe kabla kubugiwa, wanasema ni kuwaondolea mikosi wakati wanasherehekea kama vile kuumwa na tumbo.

Barobaro alipewa marufuku ya mwezi mmoja dhidi ya kujiunga na wazee hao. 

“Tumekupa adhabu ya mwezi mmoja, ujiite mkutano jinsi utakavyokuwa ukitangamana na wazee na kufuata sheria,” Mzee Joel Ndunda aliamuru, akiungwa mkono na wenzake.

Licha ya kuapa kutorudia kosa la aina hiyo, kijana huyo hakupewa fursa kujitetea ikibainika kwamba amekuwa na mazoea ya pupa. 

Isitoshe, ilifichuka kuwa ametekwa nyara na pombe kiasi cha kukosa kuenda kazini. 

Alionywa kutokana na tabia hiyo, akielezwa kwamba vikao vya wazee wakizima mwasho wa koo havimaanishi mtu awe mtumwa wa pombe. 

Aidha, wazee hutumia utangamano wao kujadiliana miradi mbalimbali ya maendeleo na uwekezaji. 

Huwa na vikao karibu kila wikendi mabaa kadhaa Thika Road. 

  • Tags

You can share this post!

Msanii Embarambamba aunganisha mashabiki mitandaoni kwa...

Mudavadi na Wetangula watakiwa kuvunja vyama vyao wajiunge...

T L