• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Wetang’ula afichua alikuwa wakili wa Atwoli punde alipofuzu

Wetang’ula afichua alikuwa wakili wa Atwoli punde alipofuzu

NA SAMMY WAWERU

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula amefichua kuhusu mteja wake wa kwanza alipohitimu kama mwanasheria chuoni.

Bw Wetangula ni wakili kitaaluma, licha ya kuwa mwanasiasa mwenye tajiriba ya muda mrefu.

Akizungumza katika Kaunti ya Bungoma mnamo Jumapili, Agosti 28, 2023 Spika Wetangula alidokeza kwamba Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (Cotu), Bw Francis Atwoli alikuwa mteja wake wa kwanza.

Alitoa ufichuzi huo katika ibada ya misa iliyohudhuriwa na Rais William Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua, miongoni mwa viongozi wengine mashuhuri serikalini na wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya.

“Ningependa kumkaribisha Mzee wetu, Francis Atwoli ambaye alikuwa mteja wangu wa kwanza wakati nikianza safari ya uanasheria awazungumzie,” Wetangula alisema akikaribisha Bw Atwoli kuhutubia wakazi wa Bungoma.

Ufichuzi wa Spika huyo ulisababisha watu kuangua kicheko, katika kilionekana kama kushangazwa na udokezi wake.

Alipochukua kipaza sauti, Katibu Mkuu huyo wa Cotu alikiri kuwa mteja wa kwanza wa Wakili Wetangula.

“Akiwa angali kijana, alikuwa akiniwakilisha katika masuala ya sheria. Nimemuona akikua,” Bw Atwoli alielezea.

Kabla kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Wetangula alikuwa Seneta wa Bungoma.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022, Atwoli aliunga mkono kuchaguliwa kwa kinara wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga.

Lakini baada ya Dkt Ruto kuapishwa kuhudumu kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya, alibadilisha msimamo wake na kuunga mkono utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Atwoli hujitambua kama nabii wa masuala ya siasa nchini, ila utabiri wake 2022 uligonga mwamba baada ya chaguo lake kuingia Ikulu – Raila Odinga kuonyeshwa kivumbi na William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Budapest 2023: Hongera Kenya kwa kuwa bingwa Afrika, na...

Raila motoni kwa kutishia kurejelea maandamano

T L