• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
Budapest 2023: Hongera Kenya kwa kuwa bingwa Afrika, na nambari 5 duniani 

Budapest 2023: Hongera Kenya kwa kuwa bingwa Afrika, na nambari 5 duniani 

NA MWANGI MUIRURI 

LICHA ya kuonekana dhaifu katika mashindano ya ubingwa wa riadha duniani yaliyoandaliwa nchini Hungary, Kenya imeibuka bora zaidi Barani Afrika kwa kujizolea medali 10.

Medali hizo zilikuwa dhahabu tatu, fedha tatu na shaba nne katika mashindano hayo yaliyodumu kuanzia Agosti 19 hadi Agosti 27, 2023.

Afrika Kusini ambayo ndiyo huonekana kama supa pawa wa Afrika, ilimaliza ikiwa hoi baada ya kuandikisha matokeo duni kabisa ya medali sufuri.

Kenya ilimaliza katika nafasi ya tano duniani.

Nafasi hiyo ilitakasa nembo ya maandalizi mabovu, siasa chafu katika wizara ya michezo na matamshi yasiyo ya kiuzalendo katika mitandao ya kijamii ambayo yaliangazia mashujaa hao wa kitaifa waliosafiri kupeperusha bendera ya taifa hili kama waliokuwa watahiniwa wa kuangukia pua.

Walioshinda dhahabu ni Faith Kipyegon katika mbio za mita 5,000 na mita 1,500, huku Mary Moraa akileta nyumbani dhahabu katika mbio za mita 800.

Beatrice Chepkoech alileta fedha katika mbio za mita 3,000 katika harakati ambazo Faith Cherotich alipata medali ya shaba huku Emmanuel Wanyonyi akiwa na miaka 19 pekee aking’arisha bendera ya Kenya kwa fedha katika mbio za mita 800.

Daniel Simiu Ebenyo alikuwa ameipa Kenya medali ya fedha katika mbio za mita 10,000, huku Jacob Krop alipata medali ya shaba katika mbio za mita 5,000.

Taifa la Ethiopia ambalo limekuwa likivizia Kenya katika riadha, liliridhika na nafasi ya pili Barani Afrika likitwaa dhahabu mbili, fedha nne na shaba tatu.

Taifa la Uganda nalo liliridhika na nafasi ya tatu Afrika kwa kutwaa dhahabu mbili katika mashindano hayo.

Morocco ilimaliza katika nafasi ya nne kwa kupata dhahabu moja na shaba moja, huku Burkina Faso ikipata dhahabu moja na kuibuka ya tano Afrika.

Botswana ikiwa ya sita, ilitwaa fedha moja na shaba moja na kufunga orodha ya mataifa ya Afrika yaliyofanikiwa kupanda jukwaa kutuzwa medali.

Amerika ilimaliza ya kwanza kwa kupata medali 29 zikiwa ni dhahabu 12, fedha nane na shaba tisa.

Canada ilikuwa ya pili kwa kupata dhahabu nne na fedha mbili, huku Uhispania ikiwa ya tatu kwa kupata dhahabu nne na fedha moja.

Taifa la Jamaica lilikuwa la nne baada ya kujizolea dhahabu tatu, fedha tano na shaba nne, na ndipo Kenya sasa ikaingia ikiwa ya tano katika usajali huo.

Nchi ya Uchina ilimaliza katika nafasi ya 37 kwa kuzoa shaba mbili pekee, Ukraine nayo ikizoa dhahabu moja na fedha moja kumaliza katika nafasi ya 14 ulimwenguni.

Qatar ambayo ina mazoea kununua Waafrika kuiwakilisha katika mashindano, ilimaliza ikiwa ya mwisho katika nafasi ya 39 kwa kupata shaba moja pekee.

[email protected]

 

Zifuatazo ni nchi 10 bora katika Mashindano ya Kimataifa ya Riadha Budapest, Hungary 2023

 

Nchi     Dhahabu    Fedha   Shaba    Jumla

USA      12                8                9           29

Canada 4                 2                 0            6

Spain     4                 1                 0            5

Jamaica 3                5                4             12

Kenya    3                3                4             10

Ethiopia 2               4                3              9

Britain    2               3                5             10

Netherlands 2       1                2             5

Norway   2              1                1             4

Sweden    2             1               0             3.

 

  • Tags

You can share this post!

Vijana wa Eldoret walioahidiwa kazi nchini Qatar wataka...

Wetang’ula afichua alikuwa wakili wa Atwoli punde...

T L