• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 3:24 PM
Wito wazazi wawafae watoto waimarike kielimu

Wito wazazi wawafae watoto waimarike kielimu

Na SAMMY KIMATU

WAZAZI wameombwa kusaidiana na watoto wao kufanya kazi ya ziada wanafunzi wanayopewa shuleni kukubatia mfumo wa mtaala mpya wa umilisi, CBC (Competence Based Curriculum).

Aidha, wazazi wameshauriwa kuhakikisha wanao wako salama nyumbani wanapokwenda kazini na kusisitizia watoto kudumisha nidhamu na maadili mema wakati wote.

Hayo yalinenwa Jumanne na mkurugenzi wa The Rock School iliyoko katika mtaa wa Hazina, South B, kaunti ndogo ya Makadara, Bi Christine Kathukya.

Bi Kathukya alisema hayo wakati wa hafla ya Siku ya Utamaduni iliyofanyika katika uga wa kanisa katoliki la St Margaret South B.

“Serikali inataka kupitia kwa mtaala mpya wa CBC wazazi kushirikiana na watoto kufanya kazi ya ziada wanapokuwa pamoja nyumbani,” Bi Kathukya akanena.

Isitoshe, alieleza kwamba kuna umuhimu wa wanafunzi kufahamu kuhusu utamaduni wa waafrika ili kujua kuna mema katika mafunzo yake.

“Ni vyema watoto kusomeshwa kuhusu vyakula vya zamani na umuhimu wake katika kuboresha afya ya binadamu maishani. Tuna vyakula kama vile maboga, viazi vitamu na mihogo miongoni mwa vingine ambayo vina rotuba katika miili yetu,” akaeleza.

Bali na hayo, watoto na walimu wao walikuwa na kipindi cha kuonyesha wazazi na wageni bidhaa walivyotengeneza baada ya mafunzo ya CBC.

Ili kuwapatia watoto na walimu motisha, wageni na wazazi walinunua bidhaa zilizotengenezwa na wanafunzi.

Walionunua na kupata fursa ya kuzungumza na Taifa Leo walisema kwa hakika watoto wana vipaji vinavyoweza kuwasaidia katika siku za usoni.

Mzazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina Bi Winnie Mulonzi alisema kuna haja ya wazazi kutambua vipaji vya watoto ndiposa vipaliliwe mapema.

“Ikiwa vipaji vya watoto vitatambuliwa mapema na rasilmali ziwepo ili talanta hizo zipaliliwe, bila shaka watoto watajifaidi binafsi sawia na kuifaidi nchi ya Kenya,” Bi Mulonzi akanena.

Kwa mfano walionyesha jinsi wanavyotengeneza vifaa vya kuchezea wakitumia vitu vinavyopatikana kwa urahisi katika mazingira wanamoishi nyumbani.

Baadhi ya walivyoonyesha wazazi na wageni ni pamoja na shanga, vitambaa vilivyotiwa nakshi, bangili na mikufu miongoni mwa vingine.

Isitoshe, wanafunzi walitumbuiza hadhara kwa kukariri mashairi, kuimba nyimbo, kusakata densi na nyimbo za kitamanduni.

Zaidi ya hayo, watoto walivalia mavazi yanayoambatana na uasilia wa nyimbo walizoimba kutokana na chimbuko la makabila mbalimbali ya Kenya.

Vilevile, mavazi waliyovalia yalikuwa yamepamwa kwa kutiwa rangi zilizokuwa na mnato na za kupendeza macho.

Kilele cha kuwatumbuiza wageni kilikuwa wakati wa kuimba nyimbo za Krismasi na kuandaa pia mchezo wa kuingiza juu ya ‘Kuzaliwa kwa Yesu’.

Waliotoa hotuba waliwauliza wazazi kutojiingiza katika makundi mabaya hasa wakati na baada ya msimu wa sherehe.

  • Tags

You can share this post!

Cindy: Sekta ya uigizaji imejaa milima na mabonde

Thika Engineers imepania kuibuka katika ligi kuu msimu ujao

T L