• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
BENSON MATHEKA: Ni hatari kuu Bunge kupoteza uhuru wake wa kikatiba kwa kuipigia serikali magoti

BENSON MATHEKA: Ni hatari kuu Bunge kupoteza uhuru wake wa kikatiba kwa kuipigia serikali magoti

NA BENSON MATHEKA

KAZI ya Bunge ni kutunga sheria na kuhakikisha kuwa serikali inatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wabunge ni wawakilishi wa watu katika jumba hilo la kutunga sheria ambalo kulingana na Katiba, linafaa kuwa huru ili liweze kupiga darubini utendakazi wa serikali.

Kenya inakumbatia demokrasia ya vyama vingi na ndiyo maana wabunge wanatoka vyama na mirengo tofauti ya kisiasa.

Kwa kuwa kazi ya Bunge ni kupiga darubini utendakazi wa serikali kuu, kuna hatari wabunge hasa wa vyama vya upinzani ‘kuwekwa makwapani’ na viongozi wa serikali.

Kuwekwa makwapani kunamaanisha kuwa demokrasia inayotarajiwa katika katiba inafifia na Bunge kupoteza mamlaka yake na kugeuka kuwa kibaraka cha serikali kuu.

Matokeo yanakuwa ni kuidhinisha sera na miswada ya serikali bila kudadisi athari zake kwa raia wanaowakilisha.

Inasikitisha kusikia wabunge wa upinzani wakitetea ukuruba wao na serikali kwa kusema wanataka maendeleo katika maeneo-bunge yao.

Hii inaonyesha kuwa viongozi hao hawafahamu majukumu yao ya kikatiba ambayo nilivyotangulia kusema, ni kutunga sheria na kuchunguza utendakazi wa serikali kuhakikisha uko chini ya Katiba.

Kwa kuonekana kupigia magoti serikali “kuomba maendeleo” wanayofaa kupata kwa kutekeleza kazi yao kisawasawa ni upotofu wa hali ya juu na kufanyia mzaha wapigakura waliowachagua ikiwa sio ‘kuwabeba ufala’ chembilecho vijana wa siku hizi.

Katiba ya Kenya 2010, inayotumika kwa sasa, inatoa mfumo wa kugawana rasilimali za serikali na kinachoenda moja kwa moja kwa maeneobunge kutoka Hazina ya Kitaifa ni pesa za Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maeneo Bunge ambazo matumizi yake yameelezwa bayana katika katiba.

Sidhani kama kuna mbunge anayeshauriana na wapigakura anaowakilisha kabla ya kuzuru ikulu ‘ili eneobunge lake lisinyimwe maendeleo’.

Ni hatari sana kwa raia Bunge likipoteza uhuru wake.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Uhuru asinyimwe pensheni kwa kujihusisha...

Zaidi ya maafisa 3 wauawa na kilipuzi

T L