• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Zogo la usimamizi wa mji wa Mtito Andei latokota upya

Zogo la usimamizi wa mji wa Mtito Andei latokota upya

NA LUCY MKANYIKA

MZOZO kuhusu usimamizi wa mji wa Mtito Andei kati ya kaunti za Taita Taveta na Makueni, umeanza kutokota upya chini ya serikali mpya za kaunti.

Hii ni baada ya Gavana wa Makueni, Bw Mutula Kilonzo, kusema hatafuata agizo la mahakama lililotaka Taita Taveta iwe ikikusanya kodi za kibiashara katika mji huo.

Mwaka 2021, Jaji Lucas Naikuni wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi iliyo Mombasa, alitoa agizo la muda kwamba Taita Taveta iendelee kukusanya kodi na kutoa leseni za kibiashara katika miji ya Mtito Andei na Mackinnon Road inayozozaniwa.

Mbali na kaunti hizo mbili, miji hiyo inazozaniwa pia na Kaunti za Kwale na Kajiado.

Hata hivyo, Bw Kilonzo amesisitiza kuwa mpaka wa kaunti yake na Taita Taveta uko katika Mto Tsavo na hivyo basi hatasalimisha hata kiasi kidogo cha Makueni kwa majirani.

“Tuliagizwa kwamba kodi ziwekwe kwenye akaunti ya pamoja na Taita Taveta. Heri nifungwe jela lakini sitakubali hilo,” akasema, alipohutubu Mukuyuni, Kaunti Ndogo ya Kaiti mapema wiki hii.

Kulingana naye, Baraza la Magavana limekubaliana na msimamo wake na atautetea hadi mahakamani.

Gavana wa Taita Taveta, Bw Andrew Mwadime, alisema atasubiri kusikia rasmi msimamo wa Baraza la Magavana.

“Niko Nairobi kwa hivyo nitajulisha Baraza kuhusu matamshi hayo ili tupate mwelekeo,” akasema.

Katika mwaka wa 2020, aliyekuwa gavana, Bw Granton Samboja, aliwasilisha ombi kwa Kamati ya Ushirikiano wa Kiserikali (IGRTC) kuhusu mzozo huo.

Kaunti hiyo ililaumu Makueni kwa kukataa kukutana ili kuwe na mashauriano.

Mzozo huo uliwasilishwa pia mbele ya Baraza la Magavana ambalo limekuwa likijaribu kutafutia suluhisho.

Utawala wa kwanza wa Kaunti ya Taita Taveta ulioongozwa na aliyekuwa gavana, Bw John Mruttu, na aliyekuwa seneta, Bw Dan Mwazo, pia ulijaribu kukusanya ushahidi uliolenga kutatua mzozo uliopo lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Katika mwaka wa 2020, Bw Samboja na Gavana wa Kajiado, Bw Joseph ole Lenku, walitia sahihi mkataba wa maelewano kuhusu kukomesha mzozo huo.

Hata hivyo, makubaliano yao yalipingwa na wakazi waliodai kuwa, sehemu ya Kaunti ya Taita Taveta ilikuwa inapeanwa kwa majirani wao.

Wakazi hao walielekea mahakamani kutaka makubaliano hayo yaharamishwe.

Suala hilo lilikuwa mojawapo ya ajenda za Bw Mwadime, alipoahidi wakati wa kampeni kwamba atatumia mamlaka yake kutafuta suluhisho la kudumu ili Taita Taveta isiendelee kupoteza mapato kutoka kwa kodi katika miji hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Korti yaagiza hoteli kulipa mfanyakazi aliyeachishwa kazi...

Mwangaza alivyojipata gizani

T L