• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:50 AM
Mwangaza alivyojipata gizani

Mwangaza alivyojipata gizani

Bi Mwangaza ambaye ni askofu wa kanisa, ametuhumiwa na wawakilishi wadi wa Bunge la Kaunti ya Meru kuwa amemtunukia mume wake mwanamuziki Murega Baicu nyadhifa kuu ikiwemo afisi ya kaunti.

Gavana huyo amedaiwa kumteua kinyume cha sheria Bw Baicu, ambaye ni mchezaji gitaa, kuongoza Huduma ya Vijana Meru mbali na kuwa balozi wa mahasla (wadhifa usio rasmi).

Bi Mwangaza na mumewe wanamiliki Kituo cha Baite TV pamoja na kanisa la Baite Family Fellowship ambapo Bi Kawira anahudumu kama askofu na mume wake kama msaidizi.

Hata hivyo, hatua ya kumshirikisha mume wake katika masuala ya uongozi wa kaunti imeonekana kuchochea uhasama kati yake na viongozi wa Meru wanaohisi kudhalilishwa.

Uhasama huu ulijitokeza hadharani Novemba wakati Mbunge wa Tigania Mashariki Bw Mpuri Aburi alimshutumu Bw Baicu kumshika mateka kiongozi huyo wa kaunti.

Bw Baicu alikuwa amedai kuwa, chanzo cha mvutano huo ni mgogoro kuhusu ajira, kandarasi za barabara na malipo anayodai Bw Aburi.

Hata hivyo, akizungumza Jumatano jioni, Bw Aburi alikanusha madai hayo akimshutumu mumewe Gavana Mwangaza kwa kumkosea heshima.

“Inawezekanaje kumiliki kampuni 12? Mume wa gavana hafahamu chochote kuhusu masuala haya. Ni Murega aliyekuwa anaitisha kampuni 12 ili tuzitumie kupitishia pesa. Nilikataa kwa sababu ni ulanguzi wa hela,” alisema Bw Aburi.

Isitoshe, gavana huyo ambaye amekuwa afisini kwa siku 113 pekee, ametuhumiwa kuwadharau na kuwadhalilisha viongozi wenzake, ikiwemo kuwafuta kazi kiholela maafisa wa kaunti.

Aidha, Bi Mwangaza ameshutumiwa kwa kuteua watu watano ambao hawajafuzu katika afisi za kaunti bila kufuata mchakato unaofaa wa kuajiri maafisa wa kaunti.

Madiwani pia wamemwangazia kwa kuwateua wafanyakazi kiholela bila kuzingatia katiba na sheria ikiwemo kuagiza wasimamizi wa wadi kutwaa majukumu ya Bodi ya Kusimamia Utoaji Huduma katika Kaunti.

Isitoshe, mswada huo unataja kuwafuta kazi viongozi wanne wa idara za kaunti kabla ya muda wao wa kandarasi kukamilika, ikiwemo kuwadharau viongozi wengine.

“Gavana amejihusisha na vitendo chungu nzima visivyofaa. Vitendo hivyo vimeiletea afisi ya gavana, bunge la kaunti na uongozi wake pamoja na wakazi wa kaunti ya Meru aibu, dhihaka na kuharibiwa jina kote nchini,” anahoji Bw Denis Kiogora.

Hatima ya gavana huyo sasa imo mikononi mwa maseneta baada ya Bunge la Kaunti ya Meru kuwasilisha kwa seneti jana mswada wa kumng’oa mamlakani.

Mnamo Jumatano, madiwani 67 kati ya 69 walipiga kura kuunga mkono mswada wa kumtimua gavana huyo, uliowasilishwa na Diwani wa Wadi ya Abogeta, ambaye pia ni Kiranja wa Wachache, Denis Kiogora.

Spika wa Seneti Amason Kingi anatazamiwa kutangaza kikao maalum ndani ya siku saba kuanzia jana Alhamisi ambapo Bunge la Kaunti ya Meru liliwasilisha mswada wa kumtimua Mwangaza.

Kwa mujibu wa Kifungu 33 cha Sheria kuhusu Serikali za Kaunti, Spika wa Seneti sasa anatazamiwa kuitisha kikao maalumu katika muda wa siku saba kujadili mswada huo.

  • Tags

You can share this post!

Zogo la usimamizi wa mji wa Mtito Andei latokota upya

WANDERI KAMAU: Maprofesa na manabii feki waadhibiwe vikali...

T L