• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Al-Shabaab wateketeza Kanisa, nyumba 8 kijijini Salama

Al-Shabaab wateketeza Kanisa, nyumba 8 kijijini Salama

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa kijiji cha Salama kilichoko Lamu Magharibi wameingiwa na hofu baada ya Al-Shabaab kuteketeza kanisa, nyumba nane na kuiba mbuzi na vifaa vya kielektroniki mnamo Jumatatu usiku.

Maafisa wa utawala waliozungumza na Taifa Leo na kudinda kutaja majina yao kwa kuhofia usalama wao wa kikazi walisema magaidi zaidi ya 30 waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki na vilipuzi, walivamia kijiji hicho majira ya saa mbili na nusu usiku wa Jumatatu na kuteketeza nyumba na kanisa hilo kabla ya kuiba mbuzi, televisheni, taa za kutumia mianzi ya jua na kuvuna mahindi mashambani kabla ya kutokomea kwenye msitu wa karibu.

“Walivamia maboma ya wakazi kati ya saa mbili na nusu na saa tano usiku, ambapo walichoma nyumba nane na Kanisa la Salama Redeemed Gospel Church. Pia walichinja wanambuzi saba na kuwaacha hapo. Waliiba mbuzi tisa waliokomaa, televisheni, unga na hata kuvuna mahindi mabichi mashambani kabla ya kutokomea msituni. Kwa sasa hali si shwari eneo hili,” akasema mmoja wa maafisa hao wa utawala.

Kuta za Kanisa la Redeemed Gospel Church lililochomwa kijijini Salama wakati wa shambulio la Al-Shabaab. PICHA | KALUME KAZUNGU

Askofu wa Kanisa la Redeemed Gospel Church lililochomwa kijijini Salama, Peter Muthengi amesema mali iliyochomwa ndani ya Kanisa hilo ni ya thamani isiyopungua Sh300,000.

“Nasikitika kwamba Kanisa limeteketezwa na piano, vipaza sauti, viti na mali nyingine nyingi imeharibika. Nimepoteza mali ya thamani ya zaidi ya Sh300,000 katika uvamizi wa usiku wa kuamkia leo. Serikali ituzingatie, hasa kiusalama hapa,” akasema Bw Muthengi.

Bw Muthengi ameiomba serikali kuimarisha usalama vijijini, akisisitiza kuwa siku za hivi karibuni wakazi wengi wamekuwa wakilala msituni ilhali wengine wakitorokea kwenye kambi ya Shule ya Msingi ya Juhudi kutokana na kuhofia usalama wao.

Baadhi ya waliozungumza na Taifa Leo walisema ilikuwa ni bahati kwamba wengi wao walikuwa hawamo ndani ya majumba yao kutokana na kwamba bado wanaishi kambini.

“Hakuna maafa kwa sababu nyumba nyingi hazina wenyewe. Wengi tunalala kambini na kurudi vijijini mchana. Ingekuwa kwamba tunalala vijijini mwetu leo tungeshuhudia maafa mengi ya uvamizi wa kigaidi,” akasema Simon Mwangi, mkazi wa Salama.

Kwingineko, taharuki imetanda kwenye vijiji vya Pandanguo na Salama kufuatia milio ya risasi na vilipuzi iliyosikika kwenye maeneo hayo usiku kucha.

Duru za walinda usalama zinasema kuwa magaidi hao wa Al-Shabaab walijaribu kuvamia na kuingia kwa lazima kwenye kambi ya Polisi wa Kukabiliana na Ghasia (GSU) eneo la Pandanguo majira ya saa nane unusu alfajiri lakini wakakabiliwa na kushindwa nguvu kabla ya kutokomea kwenye msitu wa Boni.

Nyumba mojawapo ya zile zilizoteketezwa kijijini Salama, Lamu Magharibi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Mzee wa kijiji eneo la Pandanguo, Ali Sharuti Jumanne aliambia Taifa Leo kuwa hofu iliyotanda kijijini haijawawezesha kutekeleza shughuli zao za kawaida.

“Tumesikia milio ya risasi na mabomu kuanzia saa nane unusu hadi saa tisa unusu alfajiri upande wa kambi ya GSU. Magaidi walirusha vilipuzi hata hapa mjini lakini havikutudhuru. Tuko na hofu hapa Pandanguo na pia kijiji jirani cha Jima ambako milio ya risasi ilisikika muda mrefu. Hatuwezi hata kwenda mashambani,” akasema Bw Sharuti.

Juhudi za kumpata Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono na msaidizi wake, Gabriel Kioni ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwani hawakupokea simu.

Mnamo Juni 24, 2023, vijiji vya Salama na Juhudi vilivamiwa na magaidi hao ambao waliwatoa watu, hasa wanaume kwa nyumba zao na kuwachinja huku wakiteketeza nyumba.

Jumla ya watu watano waliuawa na nyumba sita zikachomwa kwenye uvamizi wa Juni.

Mwezi Julai, mtu mmoja aliuawa na nyumba tano zikateketezwa na wapiganaji wa Al-Shabaab ambao walivamia kijiji cha Salama Block 17. Kulingana na maafisa wa utawala waliozungumza na Taifa Leo, magaidi zaidi ya 60 waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki, mapanga na visu, walivamia kijiji hicho majira ya saa nane na nusu usiku mkuu, ambapo walianza kuchoma nyumba na kuiba mali.

  • Tags

You can share this post!

Mkituruhusu kuchukua ranchi ya Giriama, tutamaliza tatizo...

Serikali ya Mung’aro yapata tiba ya kuzuia mauaji ya...

T L