• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:50 AM
AU yaunga Mkenya kujiunga na tume ya UN

AU yaunga Mkenya kujiunga na tume ya UN

Na AGGREY MUTAMBO

KENYA inakaribia kushinda kiti katika Tume ya Kimataifa kuhusu Sheria (ILC) baada ya mwaniaji wake kuungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU).

Serikali ya Kenya iliteua Prof Phoebe Okowa wa Chuo Kikuu cha Queen Mary cha jijini London, Uingereza, kuwania kiti hicho.

Iwapo ataibuka mshindi, Prof Okowa atakuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kuketi kwenye tume hiyo ya wajumbe 34.Tume hiyo ndiyo hutafiti na kuandikia Umoja wa Mataifa (UN) sheria za kimataifa.

Prof Okowa tayari anaungwa mkono na Uingereza.AU inatarajia kuwa mataifa yote 54 ya Afrika yataunga mkono Prof Okowa kwenye uchaguzi utakaofanyika Novemba katika mkutano mkuu wa UN.

“Nimefurahi kufahamishwa kwamba, AU imeniunga mkono,” akasema Prof Okowa.

Mkenya huyo anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Waafrika 12 wanaowania kiti hicho.

Afrika imetengewa viti tisa.

Prof Okowa ndiye mwaniaji pekee mwanamke kutoka Afrika.

Wawaniaji wengine kutoka Afrika ni Yacouba Cisse (Cote d’Ivoire), Aly Fall (Mauritania), Ahmed Amind Fathalla (Misiri), Charles C Jalloh (Sierra Leone), Kalaluka Likando (Zambia), Ahmed Laraba (Algeria), Clement Julius Mashamba (Tanzania), Ivon Mingashang (DRC), Hassan Chahdi Ouazzani (Morocco), Allioune Sall (Senegal), Louis Savadogo (Burkina Faso) na Mohamed Muaz Ahmed Tungo (Sudan).

Tume ya ILC iliundwa mnamo 1947 na wajumbe wanahudumu kwa kipimdi cha miaka mitano.

Mkenya mwingine, Waziri wa Kawi Dkt Monica Juma, yumo mbioni kuwania kiti cha katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola.

You can share this post!

Wanavyodumisha usafi wa mazingira kwa kutumia mifuko ya...

Mabasi yarejelea safari zao za usiku, serikali ikijikokota...

T L