• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Dawa ya dawa za kulevya ni mbwa wa kunusa – Kamishna

Dawa ya dawa za kulevya ni mbwa wa kunusa – Kamishna

NA KALUME KAZUNGU

UNUNUZI wa mbwa wa kunusa ndiyo dawa tosha ya kukabiliana na kumaliza tatizo la mihadarati Lamu.

Haya ni kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Louis Rono anayeshikilia kuwa dawa za kulevya bado ni donda sugu miongoni mwa jamii eneo hilo.

Akizungumza wakati wa kongamano lililowaleta pamoja wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa kaunti ya Lamu, wawakilishi wa serikali kuu, wakuu wa usalama, mashirika ya kijamii na viongozi wa kidini leo Jumanne, Bw Rono amesema ili Lamu iimarike kwa usalama na amani, ni jukumu la kila mmoja kushirikiana kuangamiza dawa za kulevya.

Kongamano hilo la kujadili usalama, amani, uwiano na utangamano limeandaliwa mjini Mokowe na Shirika la Search for Common Ground kupitia mradi wake unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya (EU) wa Uchaguzi Bila Balaa.

Bw Rono ameshikilia kuwa amani na utulivu hauwezi kuafikiwa kikamilifu Lamu ikiwa dawa za kulevya zitaendelea kupenya na kusambazwa kwa jamii.

Kwa mujibu wa Bw Rono, vijana wengi wameharibu uzalendo wao kwa kuelekeza fikra zao katika matumizi ya mihadarati, kuzua vurugu na kuleta wasiwasi kwa jamii.

Amewasihi viongozi wa Lamu na wahisani kushirikiana na kununua mbwa wa kunusa kusaidia walinda usalama katika vita vyao dhidi ya dawa za kulevya.

“Maafisa wetu wa usalama hawalali wakikabiliana na walanguzi na watumiaji wa dawa za kulevya. Cha kusikitisha ni kwamba licha ya juhudi zilizopo, wasambazaji wa mihadarati wamekuwa wakitumia mbinu zote kukwepa mitego ya polisi na kuwasilisha dawa za kulevya Lamu. Iwapo tutashirikiana kununua mbwa wa kunusa angalau wawili watakaotumika Lamu Mashariki na Lamu Magharibi, ninaamini hili tatizo la mihadarati litaangamizwa kabisa hapa,” amesema Bw Rono.

Kwa upande wake, Gavana wa Lamu, Issa Timamy ameahidi kushirikiana na idara ya usalama katika kukabiliana na dawa za kulevya, akiongeza kuwa yuko tayari kutoa fedha maalum kwa ununuzi wa mbwa wa kunusa kusaidia kufaulisha vita hivyo.

“Mimi ninawashukuru hawa maafisa wa usalama kwa juhudi zao kukabiliana na mihadarati Lamu. Mimi niko tayari kushirikiana nao. Wakiniambia niwasaidie kununua hivi vijibwa vya kunusa kutambua mihadarati mimi niko tayari kutoa fedha maalum kufaulisha hilo,” ameahidi Bw Timamy.

Seneta wa Lamu, Githuku Kamau naye amesema ili Lamu iwe mahali bora pa kuishi kwa amani, ni vyema suala la mihadarati likabiliwe na kuangamizwa.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: ‘Bullet ant’ akiuma sehemu...

Kocha Beldine Odemba kuongoza Rising Starlets kwenye...

T L