• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
EACC yawanyaka wanawake wanaojifanya maafisa wa serikali

EACC yawanyaka wanawake wanaojifanya maafisa wa serikali

NA SHABAN MAKOKHA 

MAAFISA wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) wamewanyaka wanawake wawili ambao wamekuwa wakijifanya ni maafisa wa serikali na kuchukua pesa kutoka kwao katika eneo la Magharibi.

Wawili hao Ruth Kaimuri na Tabitha Kwena Wangeci wamekuwa na shirika lao Multi-Agency Works and Rights Enforcement, ambalo wanatumia kuwatishia wafanyabiashara na kuwaitisha hongo.

Aidha, wanasema shirika lao linaendesha misako, kuwakamata wavunjaji sheria, kukagua bidhaa wanazouza kujua ikiwa wanafuata sheria, na pia kujua ikiwa wana leseni na wanalipa ushuru.

Walinyakwa baada ya ‘kuendesha’ msako katika sehemu kadhaa za biashara katika Kaunti ya Kakamega na kutwaa mali za wafanyaviashara huku wakiitisha hongo ya kati ya Sh20,000 hadi Sh50,000 ili kuwarudishia bidhaa badala ya “mambo kufika mbele kortini”.

Mambo yaliwaendea vibaya baada ya kuitisha hongo ya Sh50,000 kutoka kwa mmiliki wa supamaketi ndogo katika kituo cha kibiashara cha Khayega, eneobunge la Shinyalu.

Wamekuwa wakijifaya ni maafisa wa EACC, Idara ya Kupeleleza Makosa ya Jinai (DCI), Polisi na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) katika kituo cha polisi cha Khayega.

Maafisa wa EACC waliwakamata wakipokea pesa hizo kutoka kwa mlalamishi na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Khayega.

Mkuu wa Mawasiliano katika EACC Eric Ngumbi alisema matapeli wanawalaghai wafanyabiashara wengi.

“Kuna wengi wamekuwa wakilaghaiwa na watu wanaojifanya ni maafisa wa EACC na vitengo vingine muhimu vya kuzuia ufisadi na uhalifu na kuhakikisha uzingatiaji wa sheri. Ifahamike kuwa EACC haipokei hongo katika kutekeleza wajibu wake,” akasema Bw Ngumbi.

Majuma mawili yaliyopita EACC ilimkamata naibu chifu mjini Bungoma aliyeitisha hongo ili atie saini kwa stakabadhi za uhamishaji wa umiliki wa shamba kwa wanafamilia waliompoteza mpendwa wao.

Bw John Murutu, ambaye ni naibu chifu wa Sitikho alikuwa ameitisha Sh10,000 kabla ya kutia saini stakabadhi hizo.

  • Tags

You can share this post!

Sasa yametosha!

Bei ya kitunguu yapanda kwa asilimia 650

T L