• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Sasa yametosha!

Sasa yametosha!

NA MHARIRI

MANENO yao pekee yanaweza kuamua iwapo Kenya itafuata mwelekeo wa mataifa mengine yaliyosambaratika au itarejea katika nyakati za giza kama ilivyokuwa hapo awali.

Kama shirika la Nation Media Group, na kwa niaba ya Wakenya kutoka matabaka yote na miegemeo yote ya kisiasa, tunataka kuwaambia wanasiasa wetu kuwa, yametosha. Kujipiga vifua kumetosha.

Siasa hatari zimetosha. Siaza za kuzua ghasia zimetosha. Siasa za ubabe zimetosha. Siasa za misimamo mikali zimetosha.

Nchi hii ni kubwa kuwazidi, Dkt Ruto na Bw Odinga.

Lazima muache misimamo yenu mikali na kufanya jambo linalofaa, ambalo ni kurejesha amani na utulivu nchini. Zaidi ya Wakenya milioni 14 walijitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, na baadaye kurejea makwao kwa amani.

Kwa karibu mwaka mmoja baadaye, bado mnatupiana cheche za matusi hadharani, hatua inayoonyesha ukosefu wa uongozi bora.

Ninyi nyote wawili mnafahamiana vyema, kila mmoja ana nambari ya simu ya mwenzake; ni wakati mwafaka kwenu kuacha majitapo yenu na kuiokoa nchi yetu.

Kwa wakati huu, haijalishi kuhusu aliye sahihi kisheria au kimaadili ni nani. Damu ya zaidi ya Wakenya 20 ambao wamefariki katika wiki za hivi karibuni, na wengine wengi kabla yao wakipigania ukombozi wa taifa hili inatosha kuamsha dhamiri zenu.

Mrengo wa Upinzani wa Azimio la Umoja-One Kenya umekuwa ukiahidi kufanya maandamano ya amani, hata hivyo, maandamano hayo yamekuwa yakisababisha vifo, ghasia na uharibifu wa mali. Hakuna ushahidi wowote uliopo kuonyesha kuwa maandamano dhidi ya serikali yatakayoanza hapo kesho yatakuwa tofauti.

Ukweli ni kuwa, kuna kila sababu kuhofia kwamba yatakuwa makali zaidi, tukizingatia matamshi makali ambayo yamekuwa yakitolewa na kila mrengo wa kisiasa.

Ni haki ya Azimio kukongamana, kususia kazi na kufanya maandamano, lakini haki hiyo imekuwa ikiendelezwa bila kuzingatia uwajibikaji wa kisheria unaoandamana nayo, yaani kudumisha na kuzingatia amani.

Ni wakati murwa kwa Bw Odinga kukubali kuwa athari za maandamano hayo zimekuwa mbaya kwa raia kuliko mafanikio, licha ya kudai anawatetea.

Ni wakati aula kwa Azimio kutathmini mikakati mipya ya kisiasa na kuwaruhusu Wakenya wa kawaida kuendelea na shughuli zao bila usumbufu.

Kushinikiza njia hii katika mazingira ya sasa ya kisiasa kutazua madhara mengi kwa watu ambao Bw Odinga na washirika wake wanadai kuwakilisha. Utawala wa Rais Ruto, kwa upande mwingine, hauwezi kuendelea kukiuka Katiba huku nchi ikiendelea kutumbukia kwenye mizozo.

Ni ukweli kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Dkt Ruto kama rais aliyechaguliwa kihalali, na Mahakama ya Upeo ikaidhinisha ushindi huo.

Rais na washirika wake wana haki ya kumkumbusha kila mmoja kuwa walishinda uchaguzi huo na wanafaa kupewa nafasi kuitawala nchi kwa miaka mitano kabla ya uchaguzi mwingine, kama ilivyo kwenye Katiba.

Kauli hiyo, hata hivyo, inahatarisha nchi kurejea kwenye ghasia za kisiasa kama zilizoshuhudiwa baada ya Uchaguzi Mkuu tata wa 2007.

Ni muhimu kwa Serikali kusikiliza sauti nyingi zinazohitaji majadiliano zikiwemo za viongozi wa kidini na wamiliki wa biashara za kibinafsi.

Kuhusu Sheria ya Fedha, japo Rais ana jukumu la kuendesha uchumi kwa kuzingatia hali ya kifedha ilivyo, ukweli mchungu ni kuwa sheria hiyo ya kifedha inambebesha raia wa kawaida mzigo mzito zaidi katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja.

Suala lingine ambalo Rais anastahili kuzingatia ni ubunaji wa Tume ya Uchaguzi ya IEBC.

Lazima Rais Ruto na Bw Odinga waiunganishe nchi na kuacha kuielekeza katika njia ya vita na kuturejesha tena kwenye mizozo. Yametosha!

  • Tags

You can share this post!

Kane ndiye anatoshea kwa viatu vya Messi – PSG

EACC yawanyaka wanawake wanaojifanya maafisa wa serikali

T L