• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Fahamu kuhusu barabara nne zinazowatia hofu wakazi wa Lamu

Fahamu kuhusu barabara nne zinazowatia hofu wakazi wa Lamu

NA KALUME KAZUNGU

KATIKA Kaunti ya Lamu, kuna barabara nne zinazokumbukwa na waja kuwa za mikosi.

Hii ni kutokana na kwamba tangu barabara hizo zianzishwe karibu muongo mmoja uliopita zimekuwa zikitumiwa sana,iwe ni wenyeji au maafisa wa usalama kusafirisha miili ya wakazi wanaouawa kila mara na washukiwa  wa kundi la Al-Shabaab.

Miongoni mwa barabara hizo ni nne hizi ambazo kila mojawapo ina urefu upatao kilomita 15. Barabara zenyewe ni Widho-Majembeni, Juhudi-Mwembe Kuinama, Githurai-Kibaoni, na Poromoko-Mavuno.

Barabara hizi ndizo kiingilio cha pekee kwa wale wanaotaka kufikia au kutoka vijiji kama vile Juhudi, Salama, Widho, Poromoko, Kaisari, Nyatha, Marafa, Mashogoni, Mikinduni na hata msitu wa Boni.

Licha ya barabara hizi kutumiwa sana na wenyeji, hasa wakulima kusafirisha mazao yao sokoni, iwe ni Majembeni Madukani, Kibaoni, Mpeketoni Mjini na Witu, mara nyingine pia barabara hizi zimetumiwa na magaidi wa Al-Shabaab kuvifikia vijiji na kuua wakazi wasio na hatia kwa kuwachinja,kuchoma nyumba,kuharibu mali na kisha kutokomea msitu wa Boni ambao unapakana na vijiji husika.

Kati ya 2014 baada ya tukio la kwanza na kubwa la kigaidi kuwahi kutekelezwa mjini Mpeketoni na kuwaacha watu zaidi ya 100 wakiuawa, nyumba na magari kuteketezwa kwa usiku mmoja,barabara hizi nne hazijaona amani na ikiwepo ni ya muda, kwani kila mara magari na vifaru vya polisi na jeshi vimekuwa vikipitapita,iwe ni kukabiliana na magaidi au kuchukua miili ya waliochinjwa na Al-Shabaab.

Makumi ya maiti za waliouawa kinyama na Al-Shabaab yamekuwa yakisafirishwa kupitia barabara hizi nne, hali ambayo imewaacha wanaozitumia wakiwa na kumbukumbu ya kutisha kwenye akili na nyoyo zao.

Bw Samuel Ngigi, mkazi wa Salama, anasema imewawia vigumu kwao kusafiri usiku wakitumia barabara hizo,akitaja kuwa mawazo ya kuogofya hugubika nafsi zao.

“Hizi barabara zimetumiwa kupitisha maiti nyingi za wenzetu wanaouawa na magaidi kiasi kwamba tunahisi roho za waliokufa huwa zinazunguka. Kweli tunatumia barabara hizo mchana lakini bado ziko upweke mno. Ni ombi letu kwamba ipo siku viongozi wa dini wataandaa mkutano wa kuziombea barabara hizi zetu kufurusha mizimu. Twahisi mizimu ya waliokufa na miili yao kusafirishwa kupitia barabara hizi imesalia kuandama,” akasema Bw Ngigi.

Naye Moneni Katana, ambaye ni mkazi wa Poromoko, aliwasihi wazee wa jamii zinazoishi vijiji husika pia kufanya tambiko vijijini na barabarani kufurusha pepo wa mauti ambaye kila mwaka hutembelea maeneo yao.

Kulingana na Bi Katana,si jambo la kawaida kwamba kila mwaka au miezi haipiti ambapo lazima matukio ya kigaidi yatatekelezwa na miili ya wanaouawa kusafirishwa kupitia barabara hizo nne.

“Hii ina maana kwamba kila mara maiti zinaposafirishwa, pepo wa mauti anaandama kutaka maafa zaidi. Ndiyo sababu utapata Al-Shabaab wanavamia kuua Januari, Juni, Julai, Agosti, na Septemba. Wazee wetu wakija pamoja na kufanya tambiko la kufurusha zimwi hili la mauti ninaamini barabara zetu zitageuzwa ziwe za kusafirishia mazao mashambani na wala si kila mara maiti,” akasema Bi Katana.

Ikumbukwe kuwa wakati mwingine magaidi wa Al-Shabaab wamekuwa wakitumia barabara hizi kuwateka nyara wakazi na kisha kuwatembeza kilomita kadhaa wakionyeshwa maboma ya kutekeleza mauaji na kisha baadaye kuwageukia na kuwaua kwa kuwachinja au kuwapiga risasi mateka wao pia.

Kwa mfano,mnamo Septemba 20, 2023, watu wanaoshukiwa kuwa ni wapiganaji wa Al-Shabaab walimvamia bawabu wa shule ya msingi ya Majembeni, George Summit Gitocho usiku ambapo walimchukua mateka na kumtembeza karibu kilomita sita kutoka Majembeni hadi kijijini Widho-Mashambani kabla ya kumchinja.

Wakati wa tukio hilo,nyumba saba ziliteketezwa na magaidi hao.

Mnamo Novemba 25, 2023, magaidi walivamia vijiji vya Marafa na Poromoko,ambapo walimchinja na kumuua mzee wa miaka 72,Bw John Thuo kabla ya kuteketeza nyumba kumi na kisha kutokomea msitu wa Boni.

Kati ya Juni na Desemba 2023, zaidi ya watu 30 waliuawa ilhali  nyumba zaidi ya 40 na kanisa vikiteketezwa na Al-Shabaab.

Miili yote imekuwa ikisafirishwa mochari ya hospitali ya Mpeketoni kupitia barabara hizo zilizotajwa.

Kwa upande wake, Joseph Njoroge ambaye ni Mwenyekiti wa Kambi ya Wakimbizi wa kigaidi iliyoko Juhudi Primary alisema kuna mwanga wa matumaini kwamba hali ya usalama kwenye barabara hiyo itaimarika kufuatia hatua ya serikali kuanzisha kambi za walinda usalama eneo hilo.

“Twashukuru. Serikali inaendeleza upanuzi wa barabara zetu na ujenzi wa vituo vya polisi na jeshi eneo hili. Ninaamini hata upweke uliopo maeneo haya utakuwa ndoto siku za usoni,” akasema Bw Njoroge.

Mapema Desemba 2023, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alitembelea eneo la Juhudi na kuamuru kambi za walinda usalama kuanza kujengwa kudhibiti hali eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Barabara iliyo kumbukumbu ya mauti, vilio katika kaunti ya...

Ruto: Nilichaguliwa kubadilisha maisha ya Wakenya, si...

T L