• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Gavana ataka bustani ya Mama Ngina sasa isimamiwe na kaunti

Gavana ataka bustani ya Mama Ngina sasa isimamiwe na kaunti

NA WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ameiomba serikali ya kitaifa iachie kaunti usimamizi wa bustani ya Mama Ngina Waterfront iliyo Likoni, na ngome ya kale ya Fort Jesus iliyo eneo la Old Town.

Bw Nassir alisema Ibara ya Nne ya Katiba ya Kenya, inazipa serikali za kaunti mamlaka ya kusimamia shughuli, sherehe na vituo vya kitamaduni ikiwemo makavazi, michezo, bustani na fuo za bahari.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa inalenga kutumia vituo hivyo vya kitalii kukuza sekta hiyo ili kupiga jeki uchumi na kuongeza nafasi za ajira miongoni mwa vijana.Awali, utawala ulioongozwa na aliyekuwa rais, Bw Uhuru Kenyatta, ulikarabati bustani ya Mama Ngina kwa Sh460 milioni na ngome ya Fort Jesus kwa Sh673 milioni ili kuvutia watalii zaidi wa kimataifa.

“Serikali ya kitaifa inafaa kurejesha usimamizi wa bustani ya Mama Ngina na ngome ya Fort Jesus chini ya serikali ya kaunti kwa mujibu wa katiba,” akasema Bw Nassir.

Hata hivyo, Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Bi Peninah Malonza, alisema atashirikiana na Bw Nassir kuhakikisha vituo hivyo viwili vya utalii vinasimamiwa na kaunti.

Hii ni baada ya Kamati ya Bunge la Kitaifa inayosimamia masuala ya Utalii na Wanyamapori kupendekeza bustani hiyo isimamiwe na kaunti kama ilivyokuwa kabla ya kupitishwa kwa katiba mpya miaka 11 iliyopita.

Wakati wa utawala wa manispaa, Mombasa ilikuwa ikisimamia vituo hivyo, lakini baada ya kupitishwa kwa katiba mpya mambo yalibadilika na serikali ya kitaifa ikachukua usimamizi wake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya seneti, Bw Kareke Mbiuki, alisema atahakikisha bustani hiyo inasimamiwa na kaunti.

Bustani hiyo iliyoko kwenye ekari 26 katika ufuo wa Bahari Hindi kando na kivukio cha feri cha Likoni huvutia maelfu ya watalii wa humu nchini na wa kimataifa.

Kwa siku, kati ya watu 400 hadi 600 huzuru kituo hicho huku wikendi kukiwa na idadi ya watu zaidi ya 1,000 wanaoitembelea.

“Tumejadiliana na Gavana Nassir kuhusu suala la kukabidhi kaunti usimamizi wa vituo vya utalii ikiwemo Mama Ngina Waterfront na ngome ya Fort Jesus na hivi karibuni tutapata suluhu kwa mujibu wa sheria zilizoko,” alisema Bi Malonza.

Waziri huyo alimpongeza gavana kwa kudumisha usafi wa mji huo wa kitalii nchini.

Hivi majuzi wasimamizi wa bustani hiyo walilalamika kuhusu kuharibika kwake baada ya watu kuanza kupatumia vibaya, na pia sehemu zake kuendelea kuwa maficho ya washukiwa wa uhalifu.

Sherehe za kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani zilikamilika Jumamosi Mombasa.Sherehe hizo ambazo ziliandaliwa katika ngome ya kale ya Fort Jesus, zilileta pamoja watalii na wapenzi wa lugha na tamaduni za Kiswahili kwa siku tatu kuanzia Ijumaa, Julai 7.

Kulikuwa na maonyesho mbalimbali ikiwemo ya vyakula vya Kiswahili, muziki, michezo na mengineyo.

Serikali ilisema inatazamia kuandaa hafla kubwa zaidi za kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani katika miaka ijayo.

Hii ilikuwa mara ya pili maadhimisho hayo kufanyika kimataifa.

  • Tags

You can share this post!

Watu 2,318 wamefariki ajalini Januari hadi sasa

Ngoi hodari wa nyimbo

T L