• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Hatua ya kuafikiana wagombeaji yazua migawanyiko

Hatua ya kuafikiana wagombeaji yazua migawanyiko

Na BARNABAS BII

MPANGO wa kugawana viti vya kisiasa katika kaunti za North Rift zenye mseto wa makabila, umeibuamivutano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Huku baadhi ya viongozi wakipendekeza mfumo huo wa demokrasia ya maelewano katika kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia, wengine wanataka wapiga kura waachiwe nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Hali ni sawa na hiyo katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet ambako makabila makuu ni Marakwet na Keiyo.

Baadhi ya wapigakura wametaja mpango huo wa kugawana viti uliopendekezwa na baadhi ya wazee wa jamii ya Kalenjin kama unaokiuka demokrasia.

Lakini kulingana na wazee hao, ugavi wa nyadhifa utasaidia kufikiwa kwa usawa wa kikabila na kimaeneo.

“Katika eneo ambako kuna makabila mengi, demokrasia ya maelewano ndio mfumo utakaohakikisha uwepo wa amani na uthabiti,” akasema Bw Kipng’etich Korir, mmoja wa wazee wa Kalenjin.

Mfumo huo ulitumika katika sehemu mbalimbali za North Rift katika uchaguzi mkuu wa 2013 licha ya kupingwa na baadhi ya wakazi.

“Hatuwezi kukubali pendekezo kama hilo kwani linahujumu misingi ya kidemokrasia kwa manufaa ya wagombeaji fulani waliopendelewa,” akasema Bw Mathew Koech kutoka Moiben, Uasin Gishu.

Haya yanajiri wakati ambapo kuna mvutano baina ya makabila mawili makuu ya Uasin Gishu kuhusu ni kabila lipi linafaa kudhamini mgombeaji wa ugavana katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Mvutano huo unahusisha makabila ya Nandi na Keiyo kuhusu linalofaa kutoa mtu wa kurithi nafasi ya gavana Jackson Mandago anayekamilisha muhula wake wa pili afisini.

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: Diana B atakiwa afute kabisa mkanda

TAHARIRI: Sharti amani idumishwe mikutano ya kisiasa leo

T L