• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
TAHARIRI: Sharti amani idumishwe mikutano ya kisiasa leo

TAHARIRI: Sharti amani idumishwe mikutano ya kisiasa leo

Na MHARIRI

JAPO mkutano wa kisiasa ambao unafanyika leo Ijumaa katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega unatarajiwa kutumika kupima ubabe wa kisiasa kati ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga na kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi eneo la Magharibi, wananchi wazilazimishwe kufuata mrengo fulani.

Aidha, wanasiasa wanaouunga mkono na wale watakaojitokeza kuupinga wasijaribu kuutumia kama kisingizio cha kuchochea uhasama miongozi mwa wananchi wa eneo hilo. Fujo zikitokea watakaoumia ni wananchi wala sio viongozi hao.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (COTU), Francis Atwoli ametangaza kuwa ajenda kuu ya mkutano huo ni kupalilia umoja kati ya jamii ya Waluhya kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Vilevile, Bw Atwoli ambaye ndiye mwandalizi mkuu wa mkutano huo, amesema kuwa mkutano huo utatoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii ya Mulembe kuelekea uchaguzi huo wa Agosti 9, 2022.

Ingawa Bw Atwoli ana haki ya kupanga mkutano kama huo, jinsi ambavyo amefanya hapo awali, hafai kuwalazimisha wananchi na viongozi wote wa eneo hili kuuhudhuria. Wajibu wake, na waandalizi wenzake, ni kutoa mwaliko kwa viongozi na wananchi kisha wakomee hapo.

Isitoshe, Katibu huyo Mkuu hana haki na mamlaka ya kuzima mikutano yoyote katika eneo la Magharibi ili kutoa nafasi kwa mkutano huo, maarufu kama Bukhungu II. Akiongea na wanahabari Jumatano, baada ya kukagua uwanja huo akiandamana na Bw Atwoli, alitangaza kuwa hakuna mkutano mwingine utakaofanyika katika kaunti za Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia leo. Alitoa wapi mamlaka ya kutoa marufuku hiyo?

Ni wakuu wa polisi eneo hilo ndio wenye mamlaka ya kufutilia mbali mikutano ya hadhara katika eneo fulani, kutokana na sababu za kiusalama.

Huenda ni matamshi kama hayo ya Bw Atwoli ndiyo yalichangia kutokea kwa kisa ambapo wazee wa jamii ndogo ya Butsotso walishambuliwa na kundi la vijana walipokuwa wakiongea na wanahabari katika mkahawa wa Golden Inn, jijini Kakamega.

Wazee hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Shiroko Shirenje walishtumu Katibu huyo Mkuu wa COTU kwamba hakutakuwa na mkutano mwingine eneo hilo leo ilhali wao hufanya hafla yao ya kitamaduni Desemba 31, kila mwaka.

Kwa upande mwingine Bw Mudavadi na kinara mwenzake wa One Kenya Alliace (OKA) Moses Wetang’ula hawafai kumshutumu Bw Atwoli kwa kuandaa mkutano wa leo. Bw Atwoli ana haki ya kuunga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja pamoja na safari ya Ikulu ya Bw Odinga.

Muhimu zaidi ni kwamba tunawahimiza wakuu wa polisi katika kaunti ya Kakamega na eneo la magharibi kwa ujumla wahakikishe kuwa amani imedumu katika mkutano wa Bukhungu II, hafla ya kitamaduni ya Butsotso na mchuano wa soka ulioandaliwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala mjini Mumias.

You can share this post!

Hatua ya kuafikiana wagombeaji yazua migawanyiko

Wasichana zaidi ya 5,000 waepuka kukeketwa, ndoa

T L