• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Wapenzi watatu wa mwanamke aliyetoweka wazungumza

Wapenzi watatu wa mwanamke aliyetoweka wazungumza

NA MWANGI MUIRURI

WANAUME watatu kati ya sita wanaohusishwa na kutoweka kwa mpenzi wao Bi Esther Ruguru mwezi Julai mwaka huu, wamejitokeza kujitetea wakisema hawana hatia.

Wachunguzi katika kesi ya Bi Ruguru, ambaye aliendesha biashara ya hoteli katika mji wa Kiria-ini, walisema alikuwa akichumbiana na wanaume sita — maafisa wawili wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), mekanika, wafanyabiashara wawili na afisa wa afya ya umma.

Hata hivyo, afisa anayesimamia uchunguzi Bw Muriithi Muriungi alisema kuwa “tumewaondoa washukiwa na kubaki na watatu wakuu — wafanyabiashara wawili na afisa wa afya ya umma.”

Wanaume hao watatu ni MaBw Boniface Macharia aliye afisa wa afya ya umma, Zablon Wambugu aliye mwanakandarasi na Stanley Maina aliye na biashara ya hoteli.

Bw Muriungi alisema watatu hao wameandikisha taarifa na wanachunguzwa “tunapotafuta kutegua kitendawili cha kutoweka kwake”.

Hayo yalijiri huku mamake Ruguru, Bi Alice Njoki, 71, akithibitisha kuwa washukiwa hao watatu walikuwa wametambulishwa kwake kama wapenzi wa binti yake.


Alice Njoki, 71, mama ya Esther Ruguru, 43, aliyetoweka mwezi Julai akizungumza nyumbani kwake katika kijiji cha Kiria, Murang’a wiki jana. PICHA | JOSEPH KANYI

Taifa Leo ilipofikia wanaume hao watatu Bw Maina alikiri kwamba “ndio tulikuwa na mipango ya kukutana na Ruguru na kwenda mjini Othaya. Lakini kabla sijamchukua nilipata ajali iliyofanya nilazwe hospitalini usiku huo.”

Hata hivyo, kadi yake ya matibabu inaonyesha kuwa alilazwa Julai 2 saa tano asubuhi wala sio usiku wa Julai 1 kama alivyodai.
Bw Macharia naye alithibitisha kwamba alikuwa akichumbiana na Bi Ruguru “lakini kwa miezi sita iliyopita tulikuwa tumekubali kuachana”.

Kwa upande wake, Bw Wambugu alisema mnamo Septemba 24 mwaka huu aliitisha mkutano wa familia nyumbani kwa Bi Njoki ili kutoa habari alizokusanya kuhusu kutoweka kwa Ruguru.

“Nilikuwa nimepata habari kwamba huenda Bi Ruguru aliuawa na kutupwa kwenye bwawa la Chinga eneobunge la Othaya,” akasema.

Aliongeza kuwa “hizi ni taarifa nilizozikusanya kutoka kwa duru za kuaminika kwani tukio hilo liliniathiri pia”.

Alisema kwamba aliitisha mkutano huo ili pia kutafuta pesa za kuwasaidia watoto watatu wa Ruguru.

Mamake Ruguru alisema bintiye, ambaye alitengana na mumewe mwaka 2015, alikuwa katika mahusiano mengine matatu ya kimapenzi na kwamba “nilifahamishwa kwa kina na binti yangu.”

Aliendelea: “Wanaume hao wote watatu walinifahamu sana kwani walikuwa wakitembea nyumbani kwangu kwa uhuru.”
Alifichua kuwa mwanzoni Ruguru aliolewa na Bw Mureithi Udi ila akarudi nyumbani na watoto wake watatu. Mumewe huyo alijiua baadaye 2017.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kupoteza Sh4.2 trilioni tabia za ushoga zikizimwa

Jinsi eneo la Kwasasi-Ingini lilivyopata jina jipya la...

T L