• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Kafyu yatangazwa vijijini kufuatia kero ya Al-Shabaab

Kafyu yatangazwa vijijini kufuatia kero ya Al-Shabaab

NA KALUME KAZUNGU

MARUFUKU ya kutotembea nje usiku imetangazwa kwenye vijiji vya Lamu ambapo mashambulio na mauaji yanayoaminika kutekelezwa na wapiganaji wa Al-Shabaab yamekuwa yakishuhudiwa.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Louis Rono alitangaza kafyu hiyo ambayo itakuwa ikianza saa moja usiku hadi saa kumi na mbili alfajiri.

Miongoni mwa vijiji ambapo kafyu hiyo inatekelezwa ni Widho, Salama, Juhudi, Marafa, Mashogoni, Ukumbi, Mavuno, Poromoko, Nyatha, Bobo-Sunkia, Safirisi na viungani mwake.

Vijiji vyote vinapatikana Kaunti Ndogo ya Lamu Magharibi.

Bw Rono alisema hatua ya kutangazwa kwa kafyu hiyo ni katika harakati za kutoa mwanya mwafaka kwa walinda usalama, ikiwemo jeshi la ulinzi nchini (KDF) na vitengo mbalimbali vya polisi kuwasaka na kukabiliana na wahalifu ambao wamekuwa wakivamia wakazi, kuwaua na kutekeleza wizi na uharibifu wa mali.

Kufikia sasa watu sita tayari wameuawa kaunti ya Lamu ilhali nyumba zaidi ya kumi zikiteketezwa moto na majangili wanaoshukiwa kuwa Al-Shabaab katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Shambulizi la hivi punde zaidi ni lile la Jumatano wiki hii ambapo magaidi waliojihami kwa silaha kali, ikiwemo bunduki, mapanga na visu walivamia vijiji vya Widho, Salama na Juhudi ambapo waliua mtu mmoja, kujeruhi askari mmoja wa akiba (NPR) na kuchoma nyumba tano.

Magaidi hao pia waliiba unga wa mahindi, ngano, mchele na mafuta na kisha kuchinja mbuzi na kubeba nyama.

Bw Rono alishikilia kuwa kutokana na utovu wa usalama unaoshuhudiwa, ni marufuku kwa wakazi wa vijiji husika kutembea usiku, hasa saa moja jioni kwendelea.

“Twataka maafisa wetu wa usalama waachwe kutekeleza kazi yao. Twataka kutumia huo usiku kuwasaka na kukabiliana na hawa wahalifu na hatutaki raia apatikane akizurura. Mtakaa ndani ya nyumba zenu kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na mbili alfajiri kwa muda au Kipindi kisichojulikana,” akasema Bw Rono.

Katika shambulizi la Jumatano, magaidi walivamia kijiji cha Salama majira ya saa nane unusu alfajiri na kuchoma mlinzi wa shamba ndani ya nyumba yake kabla ya kufululiza kwenye maboma ya kijiji jirani cha Widho ambapo walichoma nyumba nyingine nne.

Magai hao pia walivamia kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani ya shule ya Msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi, ambapo walijaribu kuilipua kwa gruneti lakini wakakabiliwa na kushindwa nguvu na maafisa wa NPR.

Mmoja wa NPR alijeruhiwa kwa risasi kwenye bega lake la kushoto wakati wa makabiliano hayo yaliyodumu kwa karibu nusu saa.

Mnamo Juni 24, 2023, magaidi zaidi ya 60 waliojihami kwa bunduki, mapanga na visu walivamia vijiji vya Juhudi na Salama, ambapo waliwashurutisha wanaume kutoka kwa nyumba zao na kisha kuwachinja.

Jumla ya wanaume watano waliuawa na nyumba sita zikiunguzwa moto wakati wa uvamizi huo uliotekelezwa kati ya saa moja unusu na saa nne usiku.

Januari, 2022, watu sita waliuawa ilhali nyumba zaidi ya kumi zikiteketezwa kwenye kijiji cha Widho, Lamu Magharibi.

Kufuatia mashambulizi hayo, serikali chini ya Waziri wa Usalama wa Ndani kwa wakati huo, Dkt Fred Matiang’i, ilitangaza kafyu kwenye vijiji husika.

Marufuku hiyo hata hivyo ilidumu kwa miei mitatu kabla ya kuondolewa Aprili, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Rais Raisi ashambulia nchi zinazolazimisha Uganda...

Raila: Wanaoambia vijana waue raia kwa mishale wakome

T L