• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Kaunti yatoa ilani kuzika miili

Kaunti yatoa ilani kuzika miili

NA MERCY KOSKEI

SERIKALI ya Kaunti ya Nakuru imetoa ilani ya siku 21 kuzika miili 17 iliyohifadhiwa katika Hifadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Nakuru kwa muda mrefu.

Katika barua iliyotumwa kwa Kamishna wa Kaunti na wasimamizi wa hospitali hiyo, kupitia afisa Mkuu wa Afya ya Umma Bi Florence Basweti, ilisema kuwa miili hiyo imesalia bila kudaiwa kwa zaidi ya miezi sita.

Kulingana na barua hiyo, maiti hizo za watu wazima zimekawia kuchukuliwa na kusababisha msongamano katika kituo hicho.

Ilibainisha kuwa wasimamizi hao wametumia mbinu zote kutafuta jamaa zao bila mafanikio, ikiongeza kuwa baada ya majuma matatu, bila mafanikio itachukua hatua ya kuzika miili hiyo.

Barua hiyo pia ilitumwa kwa Afisa wa Afya ya Umma wa Kaunti, Msajili wa Vizazi na vifo, Hakimu Mkazi wa mahakama ya Nakuru na Kamanda wa Polisi wa Kaunti.

Hii ni kulingana na sheria ambayo inataka serikali ya kaunti kufanya hivyo kabla ya kufanya uamuzi wowote kuzika miili.

“Miili hii imekuwa katika chumba cha kuhifadhi maiti kwa zaidi ya miezi mitatu na iko katika hali mbali,” barua hiyo inaeleza.

Sheria ya Afya ya Umma Sura ya 242 ya 1991 inasema kwamba mwili ambao haujadaiwa unapaswa kuondolewa kutoka kwa chumba cha kuhifadhia maiti ndani ya siku kumi na nne, ikishindikana ‘utatupwa’ kwenye kaburi la pamoja baada ya afisa wa umma kupata kibali kutoka kwa mahakama.

Kulingana na afisa wa afya ya umma kaunti ya Nakuru George Gachomba, miili hiyo imeoza huku wengi wao wakiwa waathiriwa wa ajali na wagonjwa ambao hawana vitambulisho hivyo kuwa vigumu kutafuta jamaa zao.

Bw Gachomba alisema kando na kuleta msongamano kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, pia inagharimu serikali ya kaunti pesa nyingi kuihifadhi.

Alisema mara tu mahakama itakapotoa kibali kuzika miili ambayo haijadaiwa, wataizika katika makaburi ya Nakuru Kusini.

“Nakuru ikiwa ni barabara kuu ya kuelekea kaunti zingine, ajali inapotokea marehemu na walionusurika huishia katika hospitali zetu. Baadhi yao hufa na unakuta hawana vitambulisho hivyo kuwa vigumu kutafuta jamaa zao,” alisema.

“Tunawaomba wananchi wajitokeze na kutusaidia kutambua miili ya ndugu zao ambao huenda walipotea kwani ni ghali kuhifadhi miili hiyo,” aliongeza.

 

  • Tags

You can share this post!

Migogoro ya kisiasa kati ya magavana na manaibu wao yaenea

Wito akina mama wafanye biashara ili kujikimu

T L