• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Kivutio maarufu kwa watalii Kisumu ambacho kimegeuka Sodoma na Gomora

Kivutio maarufu kwa watalii Kisumu ambacho kimegeuka Sodoma na Gomora

NA ELIZABETH OJINA

ENEO la Hippo Point ni mojawapo ya vivutio vikubwa vya utalii jijini Kisumu.

Kwa wanaopenda kutazama jua likizama jioni na wale wanaopenda kutazama viboko wakiogelea katika Ziwa Victoria, eneo hili huwa murwa kabisa.

Ni eneo ambalo hufurika wapambe haswa nyakati za wikendi na misimu ya sherehe.

Jumamosi na Jumapili hujaa watu huku shughuli mbalimbali zikinoga.

Huku watalii wakitazama ziwa, nafasi za kibiashara pia zimechipuka.

Baadhi ya wanawake wameweka vibanda vya chakula, huku vyakula vikiuzwa ndani ya mahema karibu na ziwa.

Kuna wengine walioona fursa ya kuweka eneo la kuosha magari kwa wale wanaofika huko na magari.

Hata hivyo, Hippo Point, ambapo ni mojawapo ya fuo za umma zilizosalia katika ghuba ya Winam, inaendelea kuzorota kimaadili, kiusalama na kitabia kiasi cha kuitwa ‘Sodoma na Gomora’.

Kituo hiki ambacho ndicho rahisi zaidi kukifikia, kimegeuka kuwa eneo la unywaji pombe, wizi, ujambazi, matumizi ya mihadarati, na ukahaba.

Hippo Point, kivutio cha watalii katika Kaunti ya Kisumu ambacho kimeanza kupata sifa mbaya kikigeuka mangwe ya ulevi, dawa za kulevya na sifa nyingine zisizopendeza. PICHA | ELIZABETH OJINA

Bw Alex Omondi ambaye ni mkazi wa Dunga, anasema kwamba watembezi wanaokawia eneo hilo hadi saa za usiku wamejipata wakiibiwa mali zao za thamani.

“Eneo hilo ni hatari wakati mwingine. Vijana wa riko dogo wanaotumia pikipiki huwa na visu na huvamia watalii na kuwaibia simu, pesa na mali nyingine za thamani,” anasema Bw Omondi.

Bi Helen Apiyo, ambaye ni mwanzilishi wa shirika la Linda Kesho ambalo linashughulika na visa vya utekaji nyara wa watoto anasema kudorora kwa maadili katika eneo hili la Hippo Point kumekuwa kukifanyika kwa miaka kadhaa sasa.

“Ni eneo ambalo mihadarati imekuwa ikiuzwa na makateli, huku wasichana wachanga wakiingizwa kwenye ukahaba. Wanajisi wanadhulumu watoto wengi kwa kufanya mapenzi nao ndani ya magari,” anaeleza Bi Apiyo.

Katika kituo cha polisi, kitabu cha kuripoti matukio cha OB kimejaa ripoti za visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Afisa wa kituo hicho anasema amekuwa na wakati mgumu kukabiliana na tatizo hilo ambalo limezua mgogoro wa kijamii na kiusalama kwenye eneo hilo.

Anasema ameripoti kwa wakubwa wake lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Je, ni nani anayehusika na usambazaji wa dawa za kulevya na ni kwa nini hakuna anayeshughulikia suala hilo?

Wawekezaji katika sekta ya utalii wanaohudumu kwenye ufuo wa Ziwa Victoria wamelalamikia kukosekana kwa usawa katika utoaji leseni za uuzaji pombe wakisema wachuuzi ambao hawajadhibitiwa wanakosesha biashara hoteli halali zilizo karibu ambazo zina leseni.

Miongoni mwa biashara ambazo ziko karibu na Hippo Point ni Lapal, Yatch Club, Acropolis, na Dunga Hill Camp.

Meneja wa Acropolis Gabriel Osendo alilalamika kwamba bei ya vyakula na vinywaji katika Hippo Point ni ya chini mno, jambo linalowakosesha biashara.

“Kuna vitu vingi vinavyofanyika kinyume na sheria kwenye eneo hilo na kuhatarisha maisha ya wanaotaka kukawia hadi usiku zaidi. Huwa kuna kelele nyingi na muziki wa juu utadhani ni disko matanga,” akasema Bw Osendo.

“Kunahitaji kurejeshwe utulivu ili kuwe mahali pazuri pa kupunga unyunyu.”

  • Tags

You can share this post!

Murkomen adai mapaa yanavujisha maji JKIA kwa sababu...

Kindiki sasa abatilisha notisi zilizopandisha ada za...

T L